Simba SC yapoteza mchezo wa pili Ligi ya Mabingwa

Simba SC yapoteza mchezo wa pili Ligi ya Mabingwa

Sports / 18th February, 2023

Klabu ya Simba SC imepoteza mchezo wake wa pili wa Kundi C la Michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika (CAF CL) baada ya kufungwa mabao 3-0  na Raja Casablanca ya Morocco kwenye uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.


Katika mchezo huo mabao ya Raja AC yamefungwa na Mshambuliaji Hamza Khabba 30’ na bao la pili limefungwa na Mshambuliaji Soufiane Benjdida 82’ huku bao la tatu likifungwa na Mlinzi wa kati Ismael Mokadem 86’ kwa mkwaju wa penalti baada ya Mlinzi wa Simba SC, Joash Onyango kumzuia Mchezaji wa Raja.

Simba SC anaendelea kuburuza mkia katika Kundi C la Michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa hawana alama yoyote katika msimamo wa Kundi hilo wakati Raja wanaongoza wakiwa na alama sita, nafasi ya pili ni Horoya AC wenye alama nne na Vipers SC wana alama moja pekee.


Februari 25, 2023 Simba SC watasafiri hadi nchini Uganda kuwafuata Vipers SC kwenye mchezo wa tatu wa Kundi hilo la Michuano hiyo mikubwa barani Afrika (CAF CL), Raja AC watakuwa nyumbani nchini Morocco kucheza dhidi ya Horoya AC ya Guinea kwenye mchezo wa tatu.