MGOGORO WA UONGOZI NDANI YA CHADEMA KANDA YA KASKAZINI?

MGOGORO WA UONGOZI NDANI YA CHADEMA KANDA YA KASKAZINI?

General / 24th October, 2024









Taarifa za hivi karibuni kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) zinaashiria mgongano wa madaraka kati ya Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, na Katibu wa Kanda, Amani Golugwa. Mgongano huu umejitokeza baada ya mwenyekiti wa kanda kuitisha mkutano na waandishi wa habari, huku katibu wa kanda akitangaza kuanza kwa uchaguzi wa ndani wa chama katika kanda hiyo. Wadau wamehoji jinsi gani uchaguzi wa chama unaweza kufanyika katikati ya mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa.


Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Oktoba 23, 2024, uongozi mzima wa Wilaya ya Longido na Mkoa wa Arusha umevunjwa kwa tuhuma za utovu wa nidhamu na kukiuka maadili ya chama. Uamuzi huo ulifikiwa baada ya tukio la Oktoba 22, 2024, ambapo viongozi hao walidaiwa kushindwa kusimamia kwa haki mchakato wa uchaguzi wa ndani, na hata kuhusika na vitendo vya kihuni.


Kuvunjwa kwa uongozi huu kunatoa taswira ya mgongano wa kimkakati kati ya uongozi wa kanda unaoongozwa na Godbless Lema na maamuzi yanayotoka ofisi ya Katibu wa Kanda, Amani Golugwa. Hii inazidisha mvutano ndani ya chama, huku mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa ukiendelea.


Wakati vyama vingine vikijiandaa kwa uchaguzi huo, Chadema inaonekana kuendelea na migogoro ya ndani. Kuna wasiwasi kuwa chama hicho, ambacho kinajiita cha ukombozi, kitashindwa kufikia malengo yake kama hakiwezi kushughulikia migogoro yake ya ndani. Pia, kuna hofu kwamba chama hicho kinaweza kuanza kuilalamikia serikali baada ya kushindwa kwenye uchaguzi huku matatizo ya ndani yakichangia kushindwa huko.