GSM yajiondoa udhamini mwenza NBC Premier league
Uongozi wa kampuni ya GSM leo umetangaza rasmi kujiondoa kwenye nafasi ya kuwa mdhamini mwenza wa NBC Premier league. Sababu kubwa ikiwa ni Bodi ya Ligi pamoja na Shirikisho la Soka Nchini (TFF) kushindwa kutimiza baadhi ya masharti ya mkataba uliokubaliwa na pande zote mbili.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo, Afisa wa Habari wa GSM, Allan Chonjo amesema GSM ilishawishika kuwa mdhamini mwenza wa ligi kuu ya NBC ili kukuza sekta ya mpira nchini na michezo kwa ujumla;
“Milango ya michezo ipo wazi kwa wadau wa michezo kwa kuendelea kushirikiana nasi na katika kuendeleza tasnia hii na michezo mingine kwa manufaa ya taifa letu” alisema Chonjo
Mbali na hayo Chonjo alisema kwa niaba ya Ghalib Said Mohamed ambaye ni Mwenyekiti na Mjumbe wa Kamati ya Ushindi ya Timu ya Taifa (Taifa Stars) ameamua kujiuzulu nafasi ya Uenyekiti pamoja na Mjumbe wa Kamati hiyo kuanzia leo.
Chonjo amewashukuru wadau wote na vilabu vyote kwa kuwa pamoja katika kuendeleza sekta ya michezo nchini “GSM inapenda kuwashukuru TFF, Bodi ya Ligi, vilabu vyote pamoja na wadau wote kwa kuwa sehemu ya kuendeleza sekta ya michezo hapa nchini”