Zaidi ya robo tatu wenye magonjwa yasiyoambukiza hawajitambui kama wana magonjwa hayo
Na. WAF - Mwanza
Zaidi ya robo tatu ya watu wenye Magonjwa Yasiyoambukiza hususani Kisukari na shinikizo la damu hawajitambui kama wana magonjwa hayo endapo hawakwenda kupima katika vituo vya kutolea huduma za Afya.
Hayo ameyasema leo na Mkurugenzi Msaidizi-Magonjwa Yasiyoambukiza Dkt. James Kiologwe wakati akifungua mkutano mkuu wa kitaaluma wa chama cha Wafiziotherapia Jijini Mwanza.
"Eneo la kwanza la kutambua kama mtu ana Magonjwa Yasiyoambukiza kama shinikizo la juu la damu na kisukari ni kwa mfiziotherapia kisha anampeleka kwa Daktari." Amesema Dkt. Kiologwe
Dkt. Kiologwe amesema Mfiziotherapia nafasi yake inaonekana katika kuhakikisha ubora wa maisha unaimarika kwa wagonjwa wenye kisukari kwa kuhakikisha wanafanya mazoezi ya kutosha na kula kwa wakati unaostahili.
Pia, Dkt. Kiologwe amebainisha kuwa ongezeko la Vihatarishi vinavyopelekea uwepo wa Magonjwa haya ni kutoshughulisha mwili pamoja na ongezeko la ajali ambayo inahusisha mifupa mirefu (Mikono na Miguu).
"Kuna nafasi kubwa kwa Mwanamke ya kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ambapo athari yake inakwenda hadi kizazi cha tatu kama ataepuka visababishi vya magonjwa hayo ikiwemo Vilevi na matumizi ya tumbaku." Amesema Dkt. Kiologwe
Aidha, Dkt. Kiologwe ametoa wito kwa Wafiziotherapia hao kwamba, wanapoweka mikakati ya kudhibiti magonjwa hayo waiangalie jamii kwa upana wake pamoja na uwekezaji ili uweze kuwa na matokeo mazuri.
Hata hivyo, Dkt. Kiologwe amewahakikishia Wafiziotherapia hao kuwa maombi yao na changamoto zao amezichukua na kwenda kuzishughulikia kwa pamoja ili waweze kuendelea kutoa huduma iliyo bora.
Kwa upande wake Rais wa chama cha Wafiziotherapia Bw. Patrick Foster amesema baraza hilo limekuwa sehemu ya kuhamasisha na kutoa elimu katika jamii juu ya huduma za Fiziotherapia zinazotolewa nchini.
"Pia, Chama cha wafiziotherapia kinaipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kupanua wigo wa ajira katika sekta ya Afya kwa lengo la kuendelea kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi." Amesema Bw. Foster