Bima ya Afya kwa Wote Kuwawezesha Wananchi Kuwa Huru Kupata Huduma za Afya Katika Vituo Vyote Nchini

Bima ya Afya  kwa Wote Kuwawezesha Wananchi Kuwa Huru Kupata Huduma za Afya Katika Vituo Vyote Nchini

Health and Relationships / 7th January, 2023

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Wizara ya Afya , Idara ya Kinga ,Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma , Dkt.Tumaini Haonga amesema Bima ya Afya kwa Wote itawezesha wananchi kuwa na uhuru wa kupata huduma za matibabu katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya hapa nchini.

Dkt.Haonga amebainisha hayo Jijini Mwanza ikiwa ni katika hatua za uhamasishaji kwa wananchi umuhimu wa Bima ya Afya kwa wote katika utekelezaji wa agizo la katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof.Abel Makubi la kuhakikisha kila taasisi za kisekta zinakuwa na nguvu ya pamoja katika utoaji wa elimu.

Dkt.Haonga amesema wao kama Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma iliyo chini ya Idara ya Kinga,Wizara ya Afya watakuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa Bima ya Afya kwa Wote.

“Bima ya afya kwa wote ,Wananchi wanakuwa na uhuru wa kupata huduma zote za matibabu ngazi ya zahanati hadi taifa,jambo hili litaleta ukombozi katika masuala ya kupata haki za matibabu ,sisi kama Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma tutafanya kila jitihada kutoa elimu kwa njia ya vyombo vya Habari na Mitandao mbalimbali ya kijamii “amesema Dkt.Haonga.

Aidha,Dkt.Haonga amesema Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma itaendelea kutumia mikakati ya siku zote ya kushirikisha viongozi ,watu mashuhuri,wawakilishi kutoka Makundi mbalimbali ili wananchi kupata uelewa zaidi kuhusu Bima ya Afya kwa Wote.

vlcsnap-2023-01-05-21h45m13s145

Hivyo,Dkt.Haonga ametoa wito kwa wananchi wote kuchangamkia fursa ya Bima ya Afya kwa Wote kwani itarahisisha kupata uhakika wa matibabu kabla ya kuugua.

Naye Mjumbe wa Sekretarieti ya Bima ya Afya kwa Wote kutoka Wizara ya Afya Jackline Tarimo amesema Bima ya Afya kwa Wote itarahisisha kwa mwananchi kupata matibabu bila kikwazo kwani uhalisia unaonesha kuwa kwa sasa kuna asilimia 85 ya wananchi wasiokuwa na uhakika wa kupata matibabu huku mmoja wa wananchi kutoka Mkoani Mwanza Jones Nyasome akisema akiipongeza serikali kwa kuleta Bima ya Afya kwa Wote.

Ikumbukwe kuwa Muswada wa sheria wa Bima ya Afya kwa Wote unatarajiwa kusomwa Bungeni mwishoni mwa mwezi huu Januari 2023 na iwapo utapitishwa utaanza kufanya kazi rasmi Mwezi Julai,2023 kama sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambapo Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta zimekuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa jamii ili kuwa na uelewa umuhimu wa Bima ya Afya kwa wote.