Udumavu 37.2%, Watoto chini ya Miaka mitano Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
Rosemary Senyamule, amesema kwa mwaka 2018 tafiti zimeonesha kuwa kiwango cha
Udumavu kwa watoto wenye umri wa miaka mitano katika mkoa wa Dodoma ni 37.2%,
huku watoto wenye upungufu wa uzito
wakiwa ni 17.8% na Ukondefu 3.7%.
Senyamule ameyasema hayo
leo Oktoba 18, 2022, Jijini Dodoma wakati wa zoezi la utiaji saini mikataba ya
utendaji kazi wa shughuli za lishe kati ya mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya.
“Naona utapiamlo bado
upo lakini pia udumavu ni kiashiria
kimoja kikubwa sana cha kuonesha bado tunalo tatizo, japokuwa tuliomba watu
wafanye tafiti tujue angalau hali ilivyo kwasasa au kama kuna mabadiliko kwani
takwimu tulizonazo ni zile za mwaka 2018” Amesema Senyamule.
Katika hatua nyingine, Kaimu
Afisa Lishe mkoa wa Dodoma, Adella Mlingi amesema kuwa mikataba hiyo inalengo
la kuboresha hali ya lishe na utapiamlo katika mikoa na halmashauri, kusimamia
ipasavyo utekelezaji wa afua za lishe ili kupunguza athari za udumavu na
utapiamlo kwa watoto chini ya miaka mitano pamoja na kupanga, kutenga na kutoa
fedha zote kwaajili ya kutekeleza afua za lishe katika mipango ya Halmashauri
kwa mujibu wa miongozo iliyopo.
“Kwahiyo kwa kuingia
mkataba huu, tunahakikisha kwamba halmashauri zinaweza kutekeleza afua za liche
nchini, ili mwisho wa siku kupunguza hiki kiwango cha udumavu, kiwango cha
watoto wenye uzito pungufu lakini pia ukondefu kwa watoto chini ya umri wa
miaka mitano” Amesema Mlingi.
Itakumbukwa kuwa
Septemba 30, 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluh Hassan
aliingia mikataba na wakuu wa mikoa nchini, inayohusu masuala ya lish, itakayokwenda
kutekelezwa kuanzia ngazi ya
kijiji na halmashauri.
Aidha, wito umetolewa
kwa wananchi wote kuhakikisha kuwa wanazingatia maelekezo wanayopewa na
wataalam wa lishe katika kuhakikisha wanapata lishe bora, lakini pia mama
wajawazito wanapaswa kufika mapema katika vituo vya afya, ili kupatiwa huduma
mbalimbali na watoto wapatiwe vidonge vya Vitamin A.