Dkt. Mollel awataka wadau kuwa na miradi itakayogusa wananchi moja kwa moja

Dkt. Mollel awataka wadau kuwa na miradi itakayogusa wananchi moja kwa moja

Health and Relationships / 5th July, 2022


NA WAF-MWANZA

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewaomba wadau wa maendeleo wanaotekeleza miradi mbalimbali kanda ya ziwa kupeleka fedha katika miradi itakayowagusa wananchi moja kwa moja na siyo kutumia fedha kwenye, warsha, semina na makongamano.

Dkt. Mollel amesema hayo leo wakati akiongea na wadau mbalimbali wanaofanya kazi katika mikoa ya kanda ya ziwa wakati alipokutana nao katika Hospitali ya Rufaa ya Sekoue Toure jijini Mwanza.

Dkt. Mollel amesema wadau wanatakiwa kuiga mfano wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye alitumia fedha za UVIKO-19 Shilingi trioni 1.3 kuboresha huduma mbalimbali zinazogusa wanachi nchini ikiwemo huduma za afya.

“Rais Samia alipata fedha hizo kwa ajili ya kupunguza makali ya UVIKO-19, nchi nyingi zilipata fedha hizi zikatumia kununua barakoa na mambo mengine lakini nchini kwetu Mhe. Rais ameelekeza fedha hizo kwenda kumgusa mwananchi wa kawaida huko aliko”. Amesema Dkt. Mollel.

Aidha, Dkt. Mollel amesema ameamua kuwa anakwenda kila kanda ili kukutana na wataalam wa Serikali pamoja na wadau wanaofanya shughuli za afya kuzungumza nao na kuona namna ambavyo wanaweza kuweka mikakati ya pamoja ya kugusa Maisha ya watu.

Katika mazungumzo hayo, Naibu Waziri amewaomba wadau hao kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha jamii katika uchanjaji wa chanjo ya chanjo ya UVIKO-19 ambapo wadau hao wamemuahidi Dkt. Mollel kuwa wako pamoja na Serikali katika kufikia lengo iliyojiwekea.

Pamoja na hayo Dkt. Mollel alitembelea jengo jipya linalotoa huduma za mama na mtoto katika Hospitali ya Sekou Toure na kuona jinsi huduma hizo zinavyotolewa na hakusita kuwapongeza watumishi wa Hospitali hiyo kwa huduma nzuri wanazotoa zilizopelekea kupunguza malalamiko.