Wagonjwa Nane wa Moyo, Wapandikiziwa Betri
Mkurugenzi mtendaji Hospitali ya
Benjamini Mkapa Dkt. Alphonce Chandika, amesema kuwa hospitali hiyo imefanikiwa
kutoa huduma ya kupandikiza betri kwenye moyo kwa wagonjwa nane, ambao mpaka
hivi sasa wanaendelea na majukumu yao kama kawaida.
Dkt. Chandika amesema hayo leo Oktoba
26, 2022 Jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari akieleza
kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za hospitali na utekelezaji wa bajeti
kwa mwaka wa fedha wa 2022-2023.
"Kuna
wagonjwa nane ambao mapigo yao ya moyo yanashuka sana, walihudumiwa katika
Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kupandikizwa betri kwenye moyo na kupitia
maabara hiyo tumeweza kuhudumia watoto 14 waliozaliwa na matatizo ya
moyo,"Amesema Dkt.Chandika
Hata hivyo Hospitali imeanza kufanya
upasuaji wa moyo kwa watoto wenye matatito ya kuzaliwa ya moyo, ambapo mpaka
hivi sasa tayari watoto kumi wametibiwa.
Aidha, amesema kuwa wagonjwa 39
waliobainika kuwa na matatizo makubwa ya moyo wamehudumiwa kwa kuwekewa
vipandikizi, huku wagonjwa wawili kati yao wamehudumiwa kwa dharura ambapo kama
ingekuwa ni kusafirishwa kwenda kupatiwa matibabu Dar es Salaam wangepoteza
maisha.
Pia tangu mwaka 2020, Hospitali
ilifanikiwa kuanzisha upasuaji wa nyonga na magoti kwa kuweka vipandikizi, hadi
sasa jumla ya wagonjwa 56 wamewekewa vipandikizi hivyo kwa wastani wa gharama
ya shilingi milioni 12. Gharama za huduma hii nchi za nje ni takriban milioni
35 ambapo kwa wagonjwa 56 waliohudumiwa , Serikali imeokoa jumla ya Shilingi
bilioni 1.28
"Hospitali hii ndio pekee nchini imefanikiwa kuanzisha huduma ya uvunjaji
wa mawe kwenye figo kwa kutumia mawimbi na miale pasipo kumfanyia mgonjwa
upasuaji, huduma hii imeshatolewa kwa wagonjwa 148 kwa gharama ya Shilingi milioni
1.2 kwa mgonjwa mmoja, kwa nje ya nchi gharama ni zaidi ya milioni 7 ambapo kwa
wagonjwa 148, Serikali imeokoa zaidi ya Shilingi milioni 850,"Ameeleza
Dkt.Chandika
Katika hatua nyingine, hospitali ya Benjamini Mkapa imezindua mtambo wa
kuzalisha hewa tiba ya 'Oxygen' katika ambapo
imesaidia kuokao zaidi ya milioni 500 na kuongeza mapato ya ndani ya Hospitali
kwa kukusanya zaidi ya Shilingi milioni 75 ambazo Hospitali zingine zinachangia
kwa kupelekewa huduma hiyo.
Mtambo huo una uwezo wa kuzalisha mitungi 400 ndani ya masaa 24, tangu mtambo
huu uzinduliwe, Julai 1, 2022, jumla ya mitungi 13,467 imeshazalishwa ambapo
mitungi 10,962 imetumiwa hospitali hapo na mitungi 2,505 ilisambazwa kwenye
Hospitali zenye mahitaji.