Huduma ya Afya Akili Bila Malipo Kuanzia Oktoba 7-10,2022
Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya taifa ya afya ya
akili Mirembe Dkt. Paul Lawala amesema hivi sasa kumekuwepo na matukio
mengi yanayotokea kwenye jamii yanayo sababishwa na matatizo ya afya ya
akili hali inayo pelekea kuleta madhara makubwa .
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Afya Duniani
(WHO) ya mwaka 2019, kila sekunde 40, mtu mmoja hupoteza maisha kwa
kujiua.
Katika ripoti yake ya mwaka 2022 imewahimiza
viongozi na watetezi wa afya ya akili kuongeza nguvu ,kujitolea na kuchukua
hatua ili kubadilisha mitazamo,vitendo na mbinu ya kuboresha afya ya akili
katika jamii zote, lakini pia kukabiliana na viashiria vyote vya kuondoa
unyanyapaa na kusisitiza utunzaji wa afya ya akili.
Dkt. Paul ,amezungumza hayo Oktoba 6, 2022 jijini
Dodoma wakati akiongea na waandishi wa habari kuelekea kilele cha maadhimisho
ya afya ya akili yanayoadhimishwa Oktoba 10 ya kila mwaka.
“Tunatambua kuna wingi wa matukio ambayo yapo katika
jamii yetu kwa sasa ni matukio ya kutisha pia . Ambayo yanatokea katika familia
kwa sasa haiwezi kupita wiki moja haujasikia kwamba kunatukio limetokea kwenye
jamii. Matukio ambayo kwa siku za nyuma tulikuwa hatuja yazoea sana. Na kwa
vyovyote vile matukio hayo yana sehemu moja wapo kwenye afya ya akili.’’
amesema
Kuelekea kilele hicho, amewataka wakazi wa Dodoma na
mikoa ya jirani kujitokeza kuadhimisha siku hiyo .
‘’Sisi kama hospitali tumepanga na tumeadhimisha
kutoa huduma bila malipo, huduma ya afya ya akili kwa umma kuanzia tarehe 7
Oktoba mwaka huu mpaka siku ya kilele tarehe 10 Oktoba.’’ amesema Dkt Lawala
Ameongeza kuwa, wanategemea kutoa huduma za
uchunguzi wa afya ya akili na huduma ya uchunguzi wa magonjwa mengine ya
kimwili ikiwemo shinikizo la damu.
''Pia, uzito wa mwili ,ushauri kuhusu upimaji wa
maambukizi ya virusi vya ukimwi VVU, huduma za kisaikolojia pamoja na elimu juu
ya magonjwa ya afya ya akili na athari za madawa ya kulevya.'' amesisitiza
Katika hatua nyingime, ameiomba Serikali
kuendelea kuchochea uwekezaji kwenye eneo la afya akili ,hasa kwenye eneo la
uboreshaji wa miundombinu ,upatikanaji wa dawa na vifaa tiba na
uwezeshwaji wa mafunzo ya wataalam wa afya ya akili katika ngazi ya ubingwa
na ubingwa bobezi.
“Hospitali ina wataalam bingwa wa afya ya akili wa
nne tu. Na tunakabiliwa na ukubwa wa huduma na mahitaji kwa maana ya kwamba
sasa hospitali hapa tuna wagonjwa waliolazwa 400 .Wagonjwa waliokuja kwaajili
ya kupata tiba katika mfumo wa kisheria 250 sehemu ya Isanga . Wagonjwa ambao
ni waraibu wa dawa za kulevya 500 sehemu ya Isanga. Na tuna wagonjwa 250 ambao
tunawaona kama wagonjwa wa huduma za nje.’’ amesema
Kufuatana na taarifa ya Shirika la afya Duniani
(WHO) baadhi ya magonjwa ya akili yanaanzia katika umri wa miaka 14 na
kuendelea na mengi hayabainiki, jambo ambalo linahatarisha zaidi afya ya akili.