Waziri wa afya Ummy Mwalimu atoa Maelekezo kwa MSD

Waziri wa afya Ummy Mwalimu atoa Maelekezo kwa MSD

Health and Relationships / 6th May, 2022

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu , amesema Wizara hiyo itahakikisha inafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kuifumua Bohari ya Dawa(MSD).

Pia amesema watafanyia kazi maagizo ambayo yametolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhusu bohari hiyo huku akieleza tayari amekutana na uongozi wa bohari hiyo na kutoa maelekezo kadhaa yakiwemo ya kuhakikisha dawa zinapatikana na kwa gharama nafuu.

Akizungumza leo mbele ya uongozi wa MSD, Waziri Ummy Mwalimu amesema amekuwa na kikao cha muda mrefu kati yake na MSD , hivyo kuna mambo kadhaa wamekubaliana.

“Nimekuja hapa kwa lengo la kusisitiza utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alieleza kuhusu utendaji wa MSD na akaelekeza tufanye maboresho au tuifumue.

“Kama mmefuatilia mmesikia michango ya wabunge kuhusu MSD na bahati nzuri wakati niko hapa ndani tunajaribu kuwajibishana na kufuatilia …

“Tumepata maelekezo ya Waziri Mkuu kuhusu tuhuma za ukiukwaji wa kanuni za manunuzi ambazo zinaelekeza kwa MSD.Waziri Mkuu atakuja Jumatatu kwa hiyo tusizungumze sana,”amesema Waziri Ummy

Kuhusu waliyokubaliana amesema ameelekeza kwa MSD kwamba Watanzania wanahitaji kuona bidhaa za afya zenye ubora, salama na za gharama nafuu.“Hatuhitaji taarifa za kwenye makarasati kuwa upatikanaji dawa ni asilimia 90 wakati hospitali na kwenye zahati mwananchi akienda hakuna dawa.

“Hayo ndio maelekezo ya Rais, dawa lazima zipatikane.Mtu anataka aina za bidhaa 100 lakini MSD anasema wanazo aina 35 za dawa, hivyo nimeelekeza hali hii isitokee, mtu akiagiza aina 100 za dawa angalau apate aina 90 za dawa,”amesema.

Amesema jambo la pili ambalo wamekualiana dawa na bidhaa za vifaa tiba zipatikane kwa gharama nafuu.“Kubwa ambalo nimelisisitiza ili watanzania wapate huduma bora ya dawa na vifaa tiba vyenye ubora , salama na ufanisi, la kwanza wanunue bidhaa hizi kutoka kwa wazalishaji.

“Badala ya mawakala kadri inavyowezekana na bahati nzuri sheria ya manunuzi iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016 imeeleza wazi MSD inaruhusiwa kununua dawa na vifaa tiba kutoka kwa wazalishaji

“Kwa kuzingatia mambo matatu, thamani ya fedha , ubora wa hiyo bidhaa au dawa na tatu muda wa kuifikisha hiyo dawa.Kwa hiyo tumekubaliana na MSD kununua dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji wa ndani na nje ya nchi,”amesema.

Aidha amefafanua taarifa ambazo amezipata kutoka MSD ni kwamba wanao uwezo wa kuwa na akiba ya dawa kwa mwezi mmoja, lakini Waziri Ummy Mwalimu amewataka kuwa na akiba ya dawa ya miezi minne.

“Nimewaambia kuwa na dawa za mwezi hii sitaki , hivi mahitaji ya mwezi mmoja meli ikigoma maana yake tunakosa dawa, sera inataka angalau akiba ya miezi minne, kwa hiyo kuanzia sasa hivi MSD iwe inatoa taarifa ya hali ya dawa na iwepo akiba ya miezi minne,”amesisitiza.

Amesema MSD hawana tatizo la fedha kwasababu Rais Samia na Serikali yake wamekuwa wakitoa fedha kati ya sh.bilioni 10 na Sh.bilioni 15 kwa mwezi kwa ajili ya kuiwezesha kununua dawa, hivyo hawana kisingizio.

“Jambo la tatu ambalo tumekubaliana na kusisitiza tunataka kuona maboresho makubwa eneo la wateja na shughuli za kanda zifanye maboresho,”amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Pia amesema wanataka kuona MSD inaendelea kujenga viwanda vya dawa na vifaa tiba na vilianzishwa vinakamilika na kuanza kuzalisha dawa.

“Uzalishaji wa ndani unapunguza muda wa upatikanaji dawa , pili suala la bei kuwa nafuu kwani hakutakuwa na kubadilisha fedha yetu, na tatu unajua ubora.

“Kwa hiyo tunataka kuona maboresho makubwa yakifanyika MSD.Tunafahamu MSD walipata zabuni ya kuwa wanauza dawa na vifaa tiba nchi za SADC .Tunataka kujua wameuza dawa na vifaa tiba katika nchi gani ?

kwa hiyo niseme kama Wizara ya Afya tutakeleza maelekezo ya wakuu wetu katika kufanya mapinduzi, bahati nzuri tumeshapata Mwenyekiti na Mkurugenzi.

“Lazima tufanyie kazi maelekezo ya wakuu wa nchi lakini kubwa zaidi tunataka dawa na vifaa tiba vipatikane kwenye hospitali na zahanati zetu kwa gharama nafuu,”amesema.


 Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na kutoa maelekezo kwa Menejimenti ya  Bohari ya Dawa (MSD) mbele ya Waandishi wa habari,alipokwenda kutembelea bohari hiyo leo Mei 5,2022 jijini Dar es Salaam,ambapo Waziri Ummy ameitaka MSD kuripoti hali ya upatikanaji wa dawa aina 290 kwa ajili ya matumizi angalau miezi minne na sio mwezi mmoja kama ilivyokuwa awali.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD Bwa.Mavere Tukai akieleza mbele ya waandishi wa Habari (hawapo pichani) namna alivyojipanga kuhakikisha MSD inatekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwemo na maelekezo yaliyotolewa  na Waziri katika suala zima la usambazaji na upatikanaji wa dawa kwa wananchi

Mfamasia Mkuu wa Serikali,Daudi Msasi akitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa habari

Mwenyekiti wa bodi ya Wadhamini ya MSD Bi Rosemary Silaa akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani),namna walivyojipanga na kuhakikisha MSD inatekeleza majukumu yake yote iliyopewa.