Vipodozi hatari vyauzwa Madukani
Vipodozi vyenye kemikali zenye sumu vilivyopigwa marufuku nchini vimeonekana kuuzwa waziwazi katika maduka mbalimbali pamoja na mitandao ya kijamii.
Viambata vilivyomo kwenye vipodozi hivyo, zikiwamo krimu, losheni, mafuta na sabuni za kubadilisha ya ngozi ‘skin lightening’ ni ‘Hydroquinone/ Sodium Hydroxymethylglycinate’
Baadhi ya wafanyabiashara wa vipodozi hivyo, hasa wanaouza kupitia mitandao ya kijamii ikiwamo Istagram, wanasema bidhaa hizo huondoa mabaka mwilini, kutakatisha ngozi na kuwa mweupe wa wastani, wa kati au kama mzungu kutegemeana na utashi wa mtuamiaji.
Pia, vipodozi hivyo vinaelezwa kuondoa sugu kwenye viwiko vya mkono na miguu pamoja na weusi kwenye makwapa.
Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani, Emmanuel Lugina alisema jana kuwa Sodium Hydroxymethylglycinate ni kemikali inayowekwa katika losheni, mafuta na sabuni ili kuzuia visiharibike.
“Kemikali hii ina madhara mengi, inaweza kusababisha magonjwa ya ngozi ‘allergic skin reaction’, inaweza pia kusababisha saratani ya damu (leukemia) au ya pua (nasopharyngeal carcinoma),” alisema Dk Lugina.
Hata hivyo, wiki mbili zilizopita, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lilitaja orodha ya vipodozi aina ya losheni, krimu, sabuni na maji ya kuchanganya katika losheni maarufu ‘gel’ vilivyo na viambata sumu.
TBS ilitaja aina ya vipodozi kwa kuorodhesha majina na kusisitiza kuwa, vina viambata sumu vinavyoleta madhara katika mfumo wa afya ya uzazi na saratani.
Gazeti la Mwananchi lilifanya uchunguzi katika maduka mbalimbali eneo la Kariakoo, ikiwamo Barabara ya Msimbazi na kushuhudia aina 26 za krimu na losheni 109 zilizopigwa marufuku zinauzwa kuanzia Sh15,000 mpaka Sh50,000.
Miongoni mwake ni pamoja na Exta Clear Cream, Fair&White zote, Claire Cream, Miki Beauty Cream, Clere Lemon Cream, Clare Extra Cream, Binti Jambo Cream, Body Clear Cream, Jaribu Skin Lightening Lotion na aina nyingine kadhaa za vipodozi vya kubadilisha rangi ya ngozi.
Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na gazeti hili walisema wananunua bidhaa kutoka kwa wauzaji wa jumla na hawana uelewa kuhusu bidhaa ipi ni feki.
“Kuna nyakati tunasumbuliwa kwa kuambiwa tunauza bidhaa zenye madhara kwa watumiaji, mzigo wote unachukuliwa, wao watuambie ipi na ipi haifai, tukishapata elimu hatuwezi kununua bidhaa isiyofaa na kuiweka dukani,” alisema Othman Ally, mfanyabishara wa vipodozi katika eneo hilo la Kariakoo.
“Hatuna kosa, kwani kodi tunalipa na tunafuata sheria zote.”
Mfanyabiashara wa jumla, Naomi Sanga alipoulizwa kuhusu baadhi ya bidhaa kupatikana katika duka analofanyika kazi, alisema hana taarifa kama zina madhara.
“Sisi tunauza kwa jumla. Wafanyabiashara wa mikoani wanakuja kuchukua kwetu, lakini sisi pia tunauziwa na wasambazaji,” alisema Naomi akionyesha kwamba kuna mnyororo mrefu wa uingizwaji wa bidhaa hizo nchini.
Vipodozi feki
Walipotafutwa wadau wa soko la vipodozi walisema mara nyingi wafanyabiashara wengi wamekuwa wakidurufu bidhaa China, hivyo kuzalisha za bei rahisi ukilinganisha na zile halisi ‘original’ zinazotengenezwa katika maeneo mengine.
“Wanadurufu China,” alisema mfanyabiashara maarufu wa vipodozi nchini ambaye hakutaka jina lake litajwe.
“Asilimia 90 ya vipodozi vinadurufiwa China, hakuna sehemu nyingine zaidi ya huko, wanatengeneza krimu au losheni kama zile original, wananakili kila kitu kuanzia kopo lake, sasa mtu akinunua kwangu hawezi kuona tofauti hadi hapo atakapotumia na kuona ngozi yake inachubuka au kubadilika tofauti na matarajio yake.
“Hata bidhaa zinazotoka Congo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC) chanzo ni China. Kwa sasa China imefungwa kutokana na Uviko-19, hakuna mfanyabiashara anakwenda huko bali wote wanaoagiza vipodozi wanatuma hela kwa njia ya mtandao,” alisema.
Viwanda bubu
Katika hatua nyingine, wafanyabiashara hao walitoa siri kuwa licha ya bidhaa feki kununuliwa China, pia vipo viwanda vinavyodurufu vipodozi feki ndani ya nchi, hivyo kuitaka Serikali kuchukua hatua.
“Kuna viwanda vipo wanatengeneza huko Mbagala na maeneo ya Kinondoni,” alisema Adam John, mmoja wa wafanyabiashara hao.
Mwananchi ilifanya jitihada za kwenda eneo hilo na kupiga kambi kwa siku mbili ili kubaini eneo husika palipo na kiwanda bubu, lakini hakuna taarifa zaidi zilizopatikana zaidi ya wakazi kuonyesha moja ya nyumba wakisema hawajui nini kinafanyika.
“Humo ndani hatuna taarifa sijui ni kiwanda cha kutengeneza soseji, sijui vipodozi hatuna uhakika. Ila hapa kuna watu huwa wanaingia asubuhi, wanatoka jioni hatujui wanafanya nini humo ndani. Kuna vigari vikirikuu huwa vinaingia na kutoka,” alisema mwendesha bodaboda wa eneo hilo, Juma Mhando.
Wakati hali ikiendelea kuwa si shwari katika soko la vipodozi nchini, TBS inatarajia kukutana na waagizaji, wasambazaji, wauzaji na wazalishaji wa vipodozi Mei 17 ili kujadili kwa pamoja changamoto hizo.
Meneja Uhusiano na Masoko TBS, Gladness Kaseka alisema mkutano huo unalenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu viambata sumu vilivyopigwa marufuku kutumika katika vipodozi hivi karibuni.
“Kwa mujibu wa sheria ya viwango Sura Na. 130, shirika limepewa mamlaka na wajibu wa kuchukua hatua na kudhibiti ubora wa bidhaa za aina mbalimbali na kuhimiza uzingatiaji viwango katika viwanda na biashara,” alisema Kaseka.
“Pia, kupitia sehemu ya VII ya Sheria ya Fedha Na. 8 ya mwaka 2019, shirika limepewa mamlaka zaidi ya kudhibiti usalama na ubora wa chakula na bidhaa za vipodozi.”
TBS hufanya ukaguzi kujumuisha bidhaa zote, ikiwemo vipodozi na usajili wa majengo yanayohifadhi bidhaa za vipodozi na chakula tangu ilipokabidhiwa majukumu ya kusimamia usajili wa bidhaa na majengo ya chakula na vipodozi kwa Sheria ya Fedha Na. 8 ya 2019.
Kuanzia Julai 2019 hadi Desemba 2021, ilikamata tani 54.2 za vipodozi vilivyozuiliwa (vyenye viambata sumu) vyenye thamani ya Sh591 milioni.
Hiyo ni idadi ya vipodozi vilivyozuiliwa pekee na siyo feki.