Pete za kuzuia VVU zawaibua wadau nchini

Pete za kuzuia VVU zawaibua wadau nchini

Health and Relationships / 2nd May, 2022

Wanaharakati na wataalamu wa masuala ya afya, wamesema kama Tanzania itajiridhisha kuhusu usalama na kinga dhidi ya pete maalumu ‘Dapivirine Vaginal Ring’ inayokinga Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa wanawake, iingizwe nchini ili kulinda haki ya afya kwa kundi hilo.

 

Pete hiyo inayopewa nafasi kubwa ya kushusha maambukizi kwa kundi hilo, ina madini ya silikoni inayovaliwa ukeni na hudumu kwa siku 28, huku ikitoa dawa kinga ya ‘dapivirine’ inayoua virusi hivyo ukeni.

Dawa hiyo inakuja wakati wataalamu bado wanaendelea na utafiti wa dawa ya kutibu Ukimwi.

 

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema jana kuwa kwa miaka mingi njia za kujikinga ambazo zimekuwa zikitumika zina changamoto kwa wanawake wengi, hivyo ujio wa pete hiyo utasaidia wale wanaopitia changamoto.

 

Alizitaja baadhi ya changamoto kuwa ni wanaume kutowapa uchaguzi wanawake wakati wa tendo na wao kuwa waamuzi wa nini kifanyike, hivyo wengi hushindwa hata kutumia kondomu za kike.

“Pete hizi zitasaidia watu wote, mwanamke na mwanamume ingawaje tunaona zina manufaa zaidi kwa kundi moja, itazuia pia ukatili. Hii inaweza kumsaidia mwanamke hata akibakwa itakuwa imemlinda na itasaidia kulinda haki ya afya kwa wanawake na jinsia kwa ujumla,” alisema Henga.

 

Mtaalamu wa Afya ya Uzazi kwa Vijana, Waziri Njau alionyesha wasiwasi akisema licha ya kwamba ni jambo zuri, bado malengo ya watengenezaji hayatafikiwa haraka kwa kuwa wanawake wamekuwa wagumu kutumia hata njia za uzazi wa mpango. Alitolea mfano kuhusu kondomu za kike, akisema zimekuwa zikitumika zaidi zile za kiume kwa kuwa wanawake hawana mwamko wa kujilinda wenyewe ingawaje ni wepesi kufuatilia masuala ya afya ikilinganishwa na wanaume.

 


“Hata katika takwimu wanaopima wengi ni wanawake, hasa wanapokuwa wajawazito, wanaojua hali zao za maambukizi ni wanawake, ndiyo maana wanaume hupima wanapoumwa.

 

“Nafikiri kikwazo cha kwanza kitakuwa ni kuvaa pete, sababu uzazi wa mpango wapo tayari kuweka kijiti cha miaka mitatu mpaka minne lakini si kuweka vipandikizi, wengi waoga sana katika miili yao kuingiza kitu chochote,” alisema Waziri Njau.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Dare, Dk Lilian Mwakyosi alisema, “inawezekana kukawa na kaugumu fulani kuikubali, lakini kama wataalamu tunaona ni njia sahihi, mwaka 2018 ilipokuja PrEP kulikuwa na kusuasua na ilianza kwa watu wachache kwa ufanisi mdogo, lakini kwa sasa ina asilimia 90.”