MOI yapewa siku 14 kutengeneza Mashine ya MRI na CT-SCAN

Health and Relationships / 11th May, 2022

Na.Catherine Sungura,WAF-DSM


Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi amefanya ziara ya kushtukiza Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) na kukagua mashine za MRI na CT Scan na kubaini zimeharibika.


Hata hivyo, uongozi licha ya kujua hali hiyo haukuwasilisha taarifa rasmi kwa Wizara hiyo, kutokana na hali hiyo Prof. Makubi ameagiza ndani ya siku 14 kuanzia sasa wahakikishe mashine hizo zilizonunuliwa kwa gharama kubwa na Serikali, zitengenezwe na kuanza kutoa huduma.


Prof. Makubi ameziagiza hospitali za Rufaa za Mikoa, Kanda na Taifa kuwa na mpango mbadala (Plan B) kuhakikisha wagonjwa wanaendelea kupata matibabu bila usumbufu pale mashine za Taasisi zao zinapoharibika.


"Kwa mfano hapa MOI (Plan B) yenu ni Muhimbili, wagonjwa ambao wanahitaji CT Scan na MRI wapate huduma bila kupata usumbufu na rafiki" ameagiza.


Aidha, ameziagiza ziwe na 'plan B' kwa vipimo vyote vya radiolojia na vipimo vya damu endapo itatokea changamoto wagonjwa waendelee kupata huduma.


Ameelekeza pia hospitali zote za Taifa, Kanda, Mikoa na maalum zenye mashine za kisasa kuhakikisha zinatenga asilimia kadhaa ya fedha kwa ajili ya matengenezo yake kutoka kwenye makusanyo ya ndani


Hata hivyo ameelekeza tena hospitali zote hizo kukaa na TANESCO na kufanya tathmini ya mifumo ya umeme lakini pia ziweke 'backup' ya nishati mbadala ili mifumo hiyo isiharibike pale inapotokea kukatika kwa umeme.


Vilevile amewlekeza pia kutengwa bajeti mahususi ya matengenezo na kutoa miezi mitatu (3) kuwa na mkataba wa matengenezo kwa mashine zote pamoja na vifaa vya maabara kwa hospitali zote za Rufaa za Mikoa,Kanda,Maalumu ma Taifa ili kuhakikisha zinafanyiwa matengenezo na ukarabati kwa wakati