Maofisa watano TMDA waachiwa huru
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewafutia kesi ya Uhujumu Uchumi na kuwaachia huru wafanyakazi watano wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba nchini Tanzania (TMDA) akiwemo Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula, Raymond Wigenge, waliokuwa wanakabiliwa na shtaka moja la kuisababishia hasara Mamlaka hiyo ya Sh58 milioni.
Hiyo ni baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuieleza mahakama kuwa hana nia ya kuendelea na kesi dhidi ya washtakiwa hao.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa Charys Ugullum, Ezekiel Mubito, Adelard Mtenga na Abdallah Juma.
Kwa pamoja washtakiwa hao walikuwa wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 5/2018 yenye shitaka moja la kuisababishia TMDA hasara ya Sh58, 390,000, baada ya kuidhinisha posho maalum kwa wafanyakazi ambao walishalipwa.
Washtakiwa hao wamefutiwa shtaka lao Jumanne Mei 17, 2022 chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) Sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Uamuzi wa kuwafutia kesi hiyo, umetolewa na leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Ritha Tarimo, baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.
Wakili kutoka Takukuru, Hassan Dunia aliieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya usikilizwaji ushahidi wa upande wa mashtaka lakini Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), hana nia ya kuendelea na kesi hiyo dhidi ya washtakiwa hao.
Wakili Dunia, baada ya kueleza hayo, Hakimu Tarimo alisema kupitia kifungu hicho, mahakama imewafutia shtaka washtakiwa hao na kuwaachia huru.
Hakimu Tarimo baada ya kutoa maelezo hayo, washtakiwa waliachiwa huru na kuondoka.
Tayari shahidi mmoja wa upande wa mashtaka alikuwa ameshatoa ushahidi wake dhidi ya washtakiwa hao.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani mwishoni mwa mwaka 2018 na kusomewa shtaka linalowakabili.
Hata hivyo washtakiwa wote wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, walikuwa nje kwa dhamana.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanadiawa kutenda kosa hilo kati ya Mei na Desemba 2016 katika ofisi za Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) zamani ikijulikana kama Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
Katika kipindi hicho, washtakiwa wanadaiwa katika kipindi hicho, kuisababishia hasara ya Mamlaka hiyo ya Sh58, 390,000 TMDA, baada ya kuidhinisha posho maalum kwa wafanyakazi ambao walishalipwa na kusababisha kulipwa mara mbili, wakati wakijua kuwa wafanyakazi hao walishalipwa.