Majaliwa awabana mkaguzi, mwanasheria MSD
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewabana mwanasheria mkuu na mkaguzi mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) kutokana na manunuzi yaliyokuwa yakifanywa pasipo zabuni wala mikataba kama ambavyo sheria za manunuzi zinaelekeza.
Amesema ripoti ya ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere katika bohari hiyo umeonyesha ubadhirifu mkubwa uliofanywa huku watendaji hao wakiwemo.
Majaliwa ameyasema hayo leo Jumatatu Mei 9, 2022 alipofanya ziara MSD kwa lengo la kufanya ukaguzi kutokana na watendaji kutuhumiwa kukiuka kanuni za manunuzi ya umma kama alivyoahidi siku tano zilizopita akiwa Arusha.
“Kwenye ripoti ya CAG kuna madudu mengi wewe mwanasheria (mkuu wa kitengo cha sheria MSD, Christopher Kamgisha) upo, manunuzi bila zabuni, kuna manunuzi yamefanyika bila mikataba na yamepita wewe upo kazi yako nini?” amehoji.
“Mkaguzi mkuu wa ndani (Christopher Kamgisha) unatakiwa kisaidiana moja kwa moja na Mkurugenzi Mkuu na bodi lakini hukutekeleza majukumu yako tukuache? Mbona kimya?
Waziri Mkuu: Nitakavyoona nafuu? Nakuacha sasa ili usimamie majukumu yako ipasavyo.
Hata hivyo Waziri Mkuu alisema suala hilo kwa sasa lipo chini ya Taasisi ta Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) huku akitoa angalizo kwa uongozi mpya MSD, akiwataka kuwa makini na watendaji kwani wengi hawaaminiki huku akiwataka kufanya mabadiliko ya haraka.