Madhara yatokanayo na kuacha kutumia dawa za presha

Madhara yatokanayo na kuacha kutumia dawa za presha

Health and Relationships / 30th May, 2022



Kuacha kutumia dawa za shinikizo la juu la damu (Presha) kunaweza kusababisha madhara makubwa mwilini ikiwa ni pamoja na moyo na figo kutokufanya kazi vizuri kama inavyotakiwa, ugonjwa wa kiharusi, vifo vya ghafla na misuli yad amu ya moyo kutanuka. 

 Onyo hilo limetolewa leo  na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  Peter Kisenge wakati akiongea na wananchi waliofika kupima magonjwa ya moyo na kisukari  katika hospitali ya Halmashauri ya Chalinze iliyopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni mkuu wa kitengo cha mafunzo na utafiti wa Taasisi hiyo alisema wataalamu wa JKCI wako katika hospitali hiyo kwa ajili ya kuwapima wananchi na kutoa uelewa wa magonjwa ya moyo, matumizi sahihi ya dawa za moyo  na lishe bora.

“Siku ya jana tumefanya upimaji kwa watu 185 wengi wao walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu lakini wameacha kutumia dawa kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukosa dawa, kutokuwa na uwezo wa kununua dawa na kutokuwa na uelewa wa matumizi sahihi ya dawa. Kuna ambao tumewakuta misuli yao ya damu ya moyo imetanuka hii yote ni madhara ya kuacha kutumia dawa za presha”,. 

“Tumewaanzishia dawa na kuwapa elimu ya matumizi sahihi ya dawa kwani wengi wanatumia dawa na kuziacha hawajui kuwa matumizi ya dawa za presha ni maisha pia tumewaambia madhara wanayoweza kuyapata pale watakapoacha kutumia dawa za presha”, alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge alisema huduma wanazozitoa katika upimaji huo ni za kupima urefu na uzito, kuangalia uwiano baina ya urefu na uzito, kiwango cha sukari mwilini, shinikizo la damu, kuangalia jinsi mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi na kuangalia jinsi moyo  unavyofanya kazi, kutoa elimu ya lishe bora kwa afya ya moyo na matumizi sahihi ya dawa za moyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliopata huduma hiyo walishukuru kwa huduma waliyoipata kwani wameweza kupima vipimo vya moyo, kisukari pamoja na kupewa dawa bila malipo yoyote yale.

“Nilikuwa nikilala usiku nasikia moyo wangu unadunda kwa nguvu nikapata hofu kuwa ninatatizo la moyo, baada ya kusikia wataalamu wa moyo wako hapa nimekuja kupima na kukutwa moyo wangu hauna shida ila nina tatizo la presha ambayo iko juu nimeandikiwa dawa za kwenda kutumia “, alishukuru mzee Salum Funua mkazi wa Msoga.

Juliana Selemani mkazi wa Chalinze Mbwilingu alishukuru kwa huduma aliyoipata na kusema anatatizo la presha  kwa muda wa miaka mitatu na huwa anatumia dawa lakini pale anapojisikia kuwa na naafuu anaacha kuzitumia.

“Leo hii  baada ya daktari kunifanyia vipimo amenikuta na tatizo la kutanuka kwa misuli ya moyo ameniambia tatizo hii limetokana  na kuacha kutumia dawa kwani presha imeuumiza moyo wangu. Baada ya kupewa elimu hii sintaacha kutumia dawa, ninawashauri wagonjwa wa presha kama mimi wasiache kutumia dawa hata pale wanapojiona kuwa na naafuu”, alisema Mama Juliana. 

Kwa upande wake fundi sanifu wa moyo (Technician) kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jasmine Keria alisema upimaji huo umesaidia kuweza kutumika kwa mashine nzuri na ya kisasa ya kupima mfumo wa umeme wa moyo ambayo ilikuwepo katika Hospitali hiyo.

“Hospitali hii inamashine nzuri ya kisasa ya kupima mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiogram - ECG) lakini hawakuwa wanaitumia hii ni kutokana na kutokuwa na utaalamu nayo, nimeifungua mashine hii nimeiset program na tumeitumia kuwapima wagonjwa”,. 

“Nimewafundisha jinsi ya kuitumia na hapa tulipo tunashirikina na  wataalamu wa hapa kuwapima wagonjwa kwa kufanya hivyo kutasaidia wagonjwa wanaotibiwa katika hospitali hii kuweza kupata huduma hii ya vipimo”, alisema Jasmin.

Naye Mganga mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Chalinze Dkt. Allen Mlekwa alishukuru kwa huduma inayotolewa kwa wananchi ya kupimwa magonjwa ya moyo na kisukari pamoja na wafanyakazi wa hospitali ya halmashauri hiyo kufundishwa  jinsi ya kutumia mashine ya  mfumo wa umeme na moyo pamoja na kuwapima wagonjwa.

Upimaji huo wa siku mbili unafanywa na wataalamu wa Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Halmashauri ya Chalinze iliyopo Msoga, kampuni ya dawa za binadamu ya Sunpharma ambayo inatoa dawa kwa watu wanaokutwa na tatizo la moyo, sukari, maumivu, upungufu wa damu na kampuni ya ulinzi ya K4 Security ambao wanahakikisha uwepo wa usalama kwa wananchi pamoja na mali zao.