Kampeni ya nyumba ni choo yaongeza idadi ya Kaya zenye vyoo bora nchini

Kampeni ya nyumba ni choo yaongeza idadi ya Kaya zenye vyoo bora nchini

Health and Relationships / 12th April, 2022

Imeelezwa kuwa toka kampeni ya nyumba ni choo izunduliwe mwaka 2017, imeleta matokeo chanya kwa wananchi kujenga vyoo bora na kuondokana na kujisaidia vichakani au vyoo ambavyo havistahili.

 

Hayo yamesemwa leo jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa hafla ya miaka mitano ya utekelezaji wa kampeni ya Usichukulie poa Nyumba ni Choo.

 

Waziri Ummy amesema toka kampeni hiyo iliyozinduliwa na aliyekua Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ilikua na lengo la kuhamasisha kila kaya kuwa na choo bora hadi kufikia asilimia 75 ya kaya zote nchini ifikapo Juni 2021.

 

Kampeni hiyo imeleta matokeo ambapo idadi ya kaya zenye vyoo bora imeongezeka hadi kufikia asilimia 72.1 kutoka asilimia 37.1 mwezi Desemba 2017 huku kujisaidia ovyo vichakani kumeweza kupungua kutoka asilimia 5.7 hadi kufikia asilimia 1.4.

 

“Ukiangalia katika kila kaya 100, kaya 72 zina vyoo bora lakini shirika la afya duniani (WHO) pamoja na UN wamesema lengo ni kuwa na asilimia 100 ambapo kila kaya, taasisi au sehemu zote zinazotumiwa na watu zinatakiwa kuwa na choo bora”. Amesema Waziri Ummy.

 

Aidha, Waziri Ummy amesema bado kuna tatizo la kutokua na vyoo bora katika shule nyingi nchini hivyo Wizara imejipanga kuzindua kampeni hiyo awamu ya pili ili kuhakikisha inafanya uhamasishaji kwa Viongozi na watendaji wa halmashauri kuhakikisha wanajenga vyoo bora pamoja na vifaa vya kunawa mikono.

 

Kwa niaba ya Serikali Waziri Ummy amewashukuru wadau wa maendeleo ikiwemo ubalozi wa Uingereza, Benki ya dunia, UNICEF pamoja na Wizara mbalimbali zilizoshiriki katika kutekeleza kampeni hiyo akiwemo balozi ambaye ni mwanamuziki Mrisho Mpoto aliyeshiriki kikamilifu katika uhamasishaji wa kujenga vyoo bora.