Dkt. Magembe: Msitumie mabavu toeni Elimu ya mazingira

Dkt. Magembe: Msitumie mabavu toeni Elimu ya mazingira

Health and Relationships / 16th December, 2021

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya, Dkt. Grace Magembe, ameonya na kukemea vikali tabia ya baadhi ya Maafisa Afya Mazingira, kutumia mabavu wanapotekeleza majukumu yao, badala yake wawe wanatoa elimu kwa kutumia maarifa na weledi wa kazi zao huku wakisimamia misingi ya sheria.

Magembe ametoa wito huo, wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Afya, unaoendelea jijini Dodoma, ambapo amesema, wapo baadhi ya maafisa Afya wamekuwa wakitoza faini ambazo sio Rafiki kwa wananchi lakini wengine kutumia nguvu na kufikia hatua ya kuharibu biashara za watu, “hali hii haipendezi wala haina afya kwa mustakabali wa ustawi wa watu wetu” alionya Dkt. Magembe.

“Waelimisheni watu, watu wakielimishwa wanaelewa sana, mathalani, kina Baba na Mama lishe, unahitaji nguvu kiasi gani kwenda kumwambia anapo osha vyombo atumieni maji moto ili kuepuka maradhi au wuuza Matunda kutumia karatasi laini za nailoni kufunika Matunda, fanyeni hivyo tuikinge jamii na maradhi.

"Nikiwa Mganga Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam enzi hizo, Kipindupindu hakiishi tulisimama kidete na tulifanikiwa, toka wakati huo zaidi ya miaka mitano Ugonjwa huo umepotea, hivyo dawa ni Elimu Elimu Elimu. ” alisema Dkt. Grace.

Dkt. Magembe, amesema hatua zichukuliwe kwa wale watakaokaidi maelekezo ya kitaalamu baada ya kuelimishwa, suala la ukaguzi wa maeneo ya umma kama shule, vyuo na ofisi kwa kutaja baadhi, ili kuhakikisha watoto wa shule wanasoma na kuishi katika mazingira safi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Magembe, amewataka Maafisa Afya hao, kufuatilia dalili za milipuko ya magonjwa kwenye jamii na kwenye mipaka ili kuhakikisha wananchi wanalindwa wasipate magonjwa na kushindwa kufanya kazi kujiingizia kipato, sambamba na Elimu ya kujikinga na maambukizi ya COVID-19 ikiwemo kuweka vyombo vya maji ya kunawa, uvaaji wa barakoa hasa kwenye mikusanyiko ya watu wengi, kuepuka misongamano isiyo ya lazima na kuchanja dhidi ya COVID-19

Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Afya Mazingira unafanyika jijini Dodoma, ukiwa na lengo la kujitathmini juu ya utendaji kazi.