Tuko tayari kusota kwa mguu si kuchukua ruzuku

Tuko tayari kusota kwa mguu si kuchukua ruzuku

Politics / 20th April, 2022

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema wapo tayari kusota na kutembea kwa mguu lakini hawakubali kuchukua ruzuku ya Sh110 milioni inayotolewa na Serikali kwa vyama vya siasa vinavyostahili.

 

Mbowe amesema wakichukua ruzuku hiyo watahalalisha matunda ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2020 ambao waliupinga haukuwa halali.

 

Mbowe ametoa kauli hiyo leo Jumatano Aprili 20, 2022 wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Mtaa wa Raha Square Kariakoo alipofanya ziara ya kuwatembelea ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa kampeni ya  'Join the Chain' yenye lengo la kuwahamasisha wananchi kukichangia chama hicho kwa ajili ya uendeshaji.

 

"Kila mwezi tulitakiwa tupate ruzuku ya Sh110 milioni lakini chama kimekataa, kwa sababu tukikubali tutahalalisha yaliyotokea katika Uchaguzi MKuu wa mwaka 2020 ambao haukuwa halali. Tupo tayari kutembea kwa mguu na wananchi wakatupatia Sh 100 au 1000, tuko tayari tusilipane mishahara na tukasota ili tuweke misimamo ya kuheshimiana katika demokrasia.

 

"Huu ni uamuzi mgumu kisiasa lakini hakuna jinsi na hii ndio  misimamo thabiti wa Chadema, ambayo wakati mwingine inatupa shida kubwa sana.Binafsi nimeumizwa kwa njia mbalimbali kuhusu misimamo lakini ndio siasa zangu” amesema.

 

Mbowe ambaye  kwa nyakati tofauti alikuwa akishangiliwa na wafanyabiashara waliokuwa wakimsikiliza, amesema ikitokea siku Chadema kimebadili msimamo basi kimepata uhakika wa jambo fulani linaloshughulikiwa.

 

Wafanyabiashara na wananchi mbalimbali walikokuwa wakifuatilia mkutano kampeni ya Join the Chain eneo la Kariakoo walikichangia Chadema Sh1 milioni.

 

Kuhusu madai ya Katiba mpya, Mbowe ambaye ni mbunge wa zamani wa Hai, mkoani Kilimanjaro amesema ajenda hiyo inapaswa kukamilika kabla ya mwaka 2025 na watawaamsha Watanzania kuidai.