Kikosi kazi cha Samia, MCT na LHRC mezani

Kikosi kazi cha Samia, MCT na LHRC mezani

Politics / 27th April, 2022

Katibu wa Kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia, Sisty Nyahoza ameainisha vituo vitakavyotumika kutoa maoni kuhusu maeneo tisa yaliyopendekezwa na kikosi kazi hicho.

Katika taarifa yake aliyoitoa jana, Nyahoza alisema kikosi kazi hicho kitaanza ratiba ya kupokea maoni ya wadau leo katika ukumbi wa Adam Sapi Mkwawa, ofisi ndogo ya Bunge Dar es Salaam.

Nyahoza ambaye pia ni Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, alisema leo asubuhi kikosi hicho kitapokea maoni kutoka Kituo Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), mchana watapokea ya Jukwaa la Katiba na alasiri wataalika Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Nyahoza ameziomba taasisi na wadau kwenda kutoa maoni na mapendekezo kuhusu maeneo hayo.

Aliyataja maeneo yatakayotolewa maoni na wadau hao ni mikutano ya hadhara, ya ndani ya vyama vya siasa, uchaguzi, mfumo wa maridhiano ili kudumisha haki, amani, utulivu na umoja wa kitaifa.

Mengine ni ushiriki wa wanawake na makundi maalumu katika siasa na demokrasia ya vyama vingi, elimu ya uraia, rushwa na maadili katika siasa na uchaguzi, ruzuku ya Serikali kwa vyama vya siasa, uhusiano wa siasa na mawasiliano kwa umma na Katiba mpya.

Alisema Aprili 28, mwaka huu asubuhi ni Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), mchana ni Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na alasiri ni Jumuia ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO).

Ratiba ya Aprili 29, mwaka huu, Nyahoza alisema saa tatu asubuhi Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania litatoa maoni yake, saa tano asubuhi Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na saa nane na nusu mchana ni Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT).

Alifafanua kuwa mbali na njia hizo, maoni hayo pia yatapokelewa na wadu mbalimbali kwa njia ya baruapepe, ujumbe wa WhatsApp, Sanduku la Posta na barua au nyaraka zitakazowasilishwa katika ofisi ya msajili.

“Vituo vitakavyotumika kupokea maoni ni Dodoma, katika jengo la Wizara ya Kazi Mtaa wa Nzuguni A, Dar es Salaam ni mtaa wa Shaaban Robert karibu na Shule ya Msingi Bunge na Zanzibar ni Mbweni Matrekta,” alisema.

Hatua hiyo inakuja baada ya kikosi kazi hicho kilichoundwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kukamilisha hatua ya mapendekezo ya maeneo tisa ya kufanyiwa kazi.

Kikosi kazi hicho kiliundwa baada ya mkutano wa wadau wa vyama wa siasa uliofanyika Desemba 15, mwaka 2021.

Machi 21, 2022, kikosi kazi hicho kilimkabidhi taarifa yake Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia aliwapa jukumu la kwenda kujadiliana na wadau mbalimbali pamoja na Serikali kuhusu mapendekezo ya kuboresha namna bora ya kufanya siasa na kukuza demokrasia.

Rais Samia alisema baadhi ya marekebisho yatakayofanywa yanaweza kuingia katika Katiba.