Rais Samia ataja sababu kutoelewana wabunge, wakurugenzi
Rais Samia Suluhu Hassan amesema baadhi ya viongozi katika halmashauri nchini wanashindwa kuelewana kutokana na kutofuatwa kanuni za fedha.
Rais Samia amebainisha hayo jana Alhamisi Mei 19, 2022 wakati akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Tabora katika siku yake ya mwisho ya ziara ya siku tatu mkoani humo.
Amesema kuwa kukwepwa kwa kanuni za fedha ndio kumesababisha kutokueleaa kwa baadhi ya viongozi wakiwamo wabunge na wakurugenzi wa halmashauri huku akisema dawa yake ni kufuatwa kwa kanuni hizo za fedha na migongano hiyo haitakiwepo.
Amesema ili kuepuka hali hiyo mabaraza ya madiwani yanapaswa kuchukua nafasi yake kwa kutoa maamuzi ya mambo kwenye halmashauri zao.
Rais Samia alikuwa akijibu malalamiko ya Mbunge wa Manonga, Seif Gulamali aliyemlalamikia mkurugenzi mtendaji wa halmashauri yake kuwa amekataa kutoa fedha za halmashauri Sh100 milioni kuunga mkono fedha alizotafuta kwa wafadhili Sh500 milioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Amesema kuwa alipata fedha Sh500 milioni kutoka kwa wafdhili kwaajili ya miradi ya maendeleo lakini ilitakiwa Sh100 milioni zitoke halashauri kuunga mkono fedha hizo alizozitafuta kwa wafadhili ambapo amedai kuwa mkurugenzi alikataa kutoa.