Membe arudishiwa uanachama CCM

Membe arudishiwa uanachama CCM

Politics / 1st April, 2022

Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM imemsamehe na kuwarudishia uanachama wao waliokuwa wanachama wawili wa chama hicho akiwamo Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Benard Membe.

 

Mwanachama mwingine aliyesamehewa na kurejeshewa uanachama wake ni Abdallah Maulid Diwani kutoka Zanzibar.

 

Februari 28, mwaka 2020, Kamati Kuu ya CCM chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Rais John Magufuli kilimfuta uanachama Membe.

 

Hayo yamesemwa leo Alhamis Machi 31,2022 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Shaka Hamidu Shaka mara baada ya kikao cha NEC kilichofanyika chini ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan.

 

Shaka amesema taratibu nyingine za kuwapatia kadi za uanachama zitafanyika katika maeneo mengine kama Katiba ya CCM inavyoelekeza.

 

Alipoulizwa iwapo waliwahi kuomba kusamehewa, Shaka amesema wanachama hao wamewahi kuomba kusamehewa kwa zaidi ya mara tatu ndani ya chama hicho.

 

“Na kwa nyakati tofauti walikuwa wakiomba kuonana na viongozi wa chama ili kuelezea hisia zao na utayari wao wa kurudi kuja kuungana na wanachama wenzao na watanzania wenye mapenzi mema ya nchi yao,”amesema.

 

Amesema hatimaye leo kwa kutumia ibara ya 102 kifungu kidogo cha nane wameridhiwa na kupokewa rasmi kuwa wanachama.

 

Shaka amesema kwa utaratibu wa chama  wanachama hao wanatakiwa kwenda katika matawi yao kuomba uanachama wa chama hicho ili wawe wanachama hai rasmi.