Watuhumiwa 14 Mbaroni kwa tuhuma za makosa ya matumizi mabaya ya mtandao kinyume na sheria.
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) linamshikilia ALLEN SAMWEL MHINA, Miaka 31, Mbondei, Mkurugenzi wa Mtandao wa kijamii wa U-turn Collection mkazi wa Temeke Mwembeyanga na wenzake 13 kwa tuhuma za kusambaza video katika mitandao ya kijamii kinyume na sheria ikimuonyesha mmoja wa wagonjwa aliyekuwa amelazwa wodi ya ICU Hospitali ya Taifa ya Muhimbili suala lililoleta taharuki kwa Hospitali hiyo na wafanyakazi wake.
Watuhumiwa hao walikutwa na vifaa mbalimbali vya kieletroniki vya kiuchunguzi ambavyo ni Kamera, Kalamu, Saa Funguo, Miwani, Kofia, Laptop, Memory Card ambavyo vyote vinachunguzwa. Kitendo kinachotuhumiwa kufanywa na watuhumiwa hao kililenga kudhalilisha, kutia hofu au kuleta taharuki suala ambalo linalazimisha mamkala hizi mbili za kisheria kuchunguza kwa kina suala hilo. Uchunguzi ukikamilika watafikishwa kwenye vyombo vingine vya kisheria.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum la Dar es Salaam limewakamata pia matapeli sugu wa viwanja kwa tuhuma za kujipatia Tsh. milioni 100 kwa njia ya udanganyifu wakijifanya wanamiliki na kuuza viwanja vya makazi ambavyo siyo vyao. Tukio limetokea kati ya mwezi Januari na Februali 2022.
Watuhumiwa hao 11 akiwemo mwanawake wamekamatwa maeneo ya Goba Kinondoni baada ya kuwatapeli Masista wa Kanisa Katoliki Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Maria Kipalapala Tabora. Watuhumiwa hawa nao watafikishwa kwenye vyombo vingine vya kisheria kwa hatua zaidi.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar Es Salaam bado linaendelea na operesheni kali dhidi ya vikundi mbalimbali vinavyojihusisha na uhalifu ikiwemo wizi wa Pikipiki, Bajaji na magari. Jeshi limefanikiwa kuwakamata Watuhumiwa 41 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na Pikipiki 29 za wizi za zingine zinazotumika kuwafanyia uhalifu zimekamatwa.
Jeshi la Polisi linawaomba Wananchi waendelee kutoa taarifa mbalimbali ili zifanyiwe kazi na vitendo vya kihalifu viweze kupungua.