Sabaya na wenzake 6 waachiwa huru
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imewaachia huru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita baada ya ushahidi uliotolewa na Jamhuri kugubikwa na utata, hivyo kushindwa kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa yanawakabili na kuwatia hatiani.
Mbali na Sabaya wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.
Hata hivyo Sabaya, Nyegu, Aweyo na Msuya wataendelea kubaki mahabusu katika gereza la Karanga kwa kuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.
Hukumu hiyo imetolewa leo Ijumaa Juni 10 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Patricia Kisinda aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo.
Hii ni kesi ya pili Sabaya kushinda ambapo Mei 6, 2022 na wenzake wawili Sylvester Nyegu na Daniel Mbura, walishinda rufaa iliyokuwa ikisikilizwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, waliyokata kupinga hukumu ya miaka 30 iliyokuwa imetolewa na na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Hakimu Kisinda amesema kuwa mbali na sababu hizo, mahakama imegundua kuwa hati ya mashitaka ilikuwa na mapungufu na kuwa ushahidi uliotolewa dhidi yao mahakamani hapo haujaweza kuthibitisha mashtaka hayo.