Chuo cha uongozi mahakama Lushoto chazindua baraza jipya la wafanyakazi

Chuo cha uongozi mahakama Lushoto chazindua baraza jipya la wafanyakazi

Legal / 6th May, 2022






KATIBU Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Mary Makondo ametoa pongezi kwa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kuwa ni miongoni mwa taasisi chache zinazoongoza kwa kuendesha mafunzo kwa njia ya Mtandao.

Ametoa kauli hiyo leo Mei 5, 2022 Jijini Dar es Salaam katika Taasisi ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Baraza la Nne la Chuo ambapo amesema Chuo kimekuwa kikifanya vizuri kwenye eneo la mafunzo kwa njia ya mtandao sio tu nchini bali katika ukanda wa Afrika na nje ya mipaka ya Afrika.

Mhe. Makondo alielezea kwamba katika kipindi hiki cha Mapinduzi ya Nne ya Viwanda ambapo matumizi ya TEHAMA na Akili Bandia yamezidi kushika kasi hii imetokana na ukweli kwamba Mahakama ya Tanzania ni Mhimili unaofanya vizuri sana kwenye matumizi ya TEHAMA katika utendaji kazi wa kila siku ikiwemo uendeshaji wa mashauri.

Aliendelea kwa kusema kwamba, Chuo kama wakala wa mafunzo kwa kutumia TEHAMA kupitia mfumo wa virtualcourt umeweza kuendesha mafunzo kwa zaidi ya watumishi 1500 wa mahakama za Tanzania mpaka sasa na idadi hiyo inaendelea kuongezeka. Kwa njia hii imeweza kukisaidia Chuo kuwafikia watumishi wa Mahakama popote walipo bila usumbufu wa kusafiri na njia hii imeweza kupunguza gharama za kuwalipa watumishi kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo mbalimbali.

Mhe.Makondo amesema amefarijika kwa jitihada zinazofanywa na chuo cha uongozi wa mahakama kwa kuendesha mashauri na mafunzo mbalimbali kwa kutumia mifumo ya Tehama iliyotengenezwa na wataalamu wa ndani.

"nimefarijika sana kuona chuo kimetumia mifumo wa uliojengwa na watalaamu wetu badala ya kutumia mifumo kama Microft teams , zoom hii inatuhakikishia usalama wa mifumo pamoja na kujenga uwezo wa ndani ,nitoe rai kwa chuo kuharakisha kuanzisha mafunzo ya muda mfupi ya komputa kwa wanasheria" alisema Makondo.

Aidha Mhe.Makondo amewataka wajumbe walioteuliwa katika Baraza la nne la wafanya kazi kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri kwa wafanyakazi wanaowawakilishi na siyo kuwa mizigo kwa uongozi na wafanyakazi katika kutatua kero zao.

Aidha Mhe. Makondo ameupongeza uongozi wa Chuo kwa jitihada za kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kununua viwanja jijini Mwanza na Mkoani Simiyu na kusema kwamba kufanya hivyo ni hatua kubwa kwa Chuo. Wizara inaamini kwamba uendelezaji wa viwanja hivyo utafanyika kwa haraka ili kufikisha huduma karibu na wananchi kama ilivyokusudiwa. Mhe. Makondo ameahidi kuwa Wizara anayoiongoza iko tayari kutoa ushirikiano unaostahili kwa Chuo wakati wowote watakapouhitaji.

Katika hafla hiyo ya uzinduzi Mhe. Makondo ametoa wito kwa waajiri wote wanaoajiri wanasheria katika utumishi wa umma kuwapeleka watumishi hao kupata mafunzo katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa mujibu wa matakwa ya Waraka wa Katibu Mkuu Ofisi ya Raisi Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Waraka Namba 5 wa mwaka 2012.

Kwa upande wake Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Mhe.Dkt. .Paul Kihwelo amesema kuwa kwa a kanuni ya 108 ya sheria za utumishi wa umma 2003 kanuni zinaelekeza kuwepo kwa chombo ambacho kitahakikisha kuwepo kwa mahusiano mazuri kazini pamoja na kuhakisha masilahi ya watumishi yanazingatiwa kwa mjibu wa sheria.

Mhe. Dkt. Kihwelo aliendelea kwa kusema wajibu wa Chuo ni kuwajengea uwezo watumishi wa mahakamama kwa kada mbalimbali Tanzania ili kuboresha utendaji wa kazi kwa maafisa.

Hafla hiyo ya uzinduzi ilikamilika kwa wajumbe kupewa mafunzo ya siku moja ya Haki na Wajibu wa Mtumishi wa Umma pamoja na Maadili ya Utumishi wa Umma mafunzo ambayo yameendeshwa na wawezeshaji wabobezi kutoka Ofisi ya Raisi Menejimenti ya Utumishi ya Umma kwa lengo la kuleta tija kwa watumishi, taasisi na taifa ili kuweza kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza katika utumishi wa mma kwakuwa Baraza la wafanyakazi ni kioo na mwanga wa taasisi.