Hatima ya Sabaya na wenzake leo

Hatima ya Sabaya na wenzake leo

Legal / 10th June, 2022

Hatima ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi inatarajiwa kujulikana leo.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha iliyokuwa ikisikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27/2021 imepanga kwa mara ya pili kutoa hukumu hiyo.

Awali, Mei 31 mwaka huu Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Patricia Kisinda aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo, alipanga kutoa hukumu lakini ilishindikana kutokana na kudaiwa kuwa nje ya kituo cha kazi kwa majukumu mengine.

Sabaya na wenzake walikuwa wakisubiri hukumu hiyo endapo wangeachiwa huru au la, kabla ya kufunguliwa kesi nyingine na wenzake watano ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Juni Mosi mwaka huu.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Fadhil Mbelwa akiahirisha kesi hiyo Mei 31 mwaka huu alisema hakimu aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo amepangiwa majukumu mengine nje ya kituo cha kazi hivyo hukumu hiyo itatolewa leo.

Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa baada ya kesi hiyo kusikilizwa kwa miezi saba tangu ilipoanza Julai, 2021.

Sabaya alikamatwa Mei 27, mwaka jana Wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam na kufikishwa mahakamani Juni 4, 2021 na kufunguliwa kesi mbili tofauti.

Katika kesi ya kwanza walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, hukumu ambayo Mei 6, 2022 ilitenguliwa na Mahakama Kuu na kuwaachia huru baada ya kubaini dosari.