Wafanyabiashara wahimizwa kuzingatia ubora wa uzalishaji bidhaa ili kukidhi viwango vya kimataifa
Mkurugenzi wa Biashara
wa Jumuisha ya Afrika Mashariki (EAC), Rashid Kibowa amesema kuwa moja ya
changamoto inayowakabili wafanyabiashara wa EAC ni kuzalisha bidhaa zenye ubora
wa chini.
Kauli hiyo ameitoa
jana Oktoba 20 jijini Dar es Salaam wakati wa utoaji wa tuzo za ubora za Afrika
Mashariki kwa mwaka 2022, hafla ambayo imefanyika katika hoteli ya four point.
Amesema changamoto
hiyo inafanya biashara za wafanyabiashara wengi katika ukanda huu zisivuke
mipaka ya jumuiya hiyo na hivyo kushindwa kushindana na wafanyabiashara wengine
wa Afrika na kimataifa.
“Tunatakiwa
kujiimarisha ili kushindana na watu wengine duniani,” amesema Kibowa.Kibowa
amesema kuna muamko mkubwa wa wajasiriamali kuzalisha bidhaa ili kujipatia
kipato lakini wengi wao hawana ujuzi na maarifa yanayowawezesha kuzingatia
viwango vya ubora vya kimataifa.
Amesema
Wafanyabiashara Afrika Mashariki wanatakiwa kuzalisha bidhaa na kutoa huduma
zenye ubora na viwango ili kufaidika zaidi na soko la kimataifa lenye faida
lukuki.
Aidha amesema Miongoni
mwa masoko muhimu la kimataifa kwa wajasiriamali ni Eneo la Biashara Huria la
Afrika (AfCFTA) ambalo ni makubaliano ya biashara huru ya Afrika kati ya nchi
54 wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).
Kutokana na hali hiyo,
nchi za EAC zinaagiza zaidi bidhaa mbalimbali kutoka nje na kulazimika
kusafirisha malighafi kama mazao ya kilimo ili yakachakatwe nje na kurejeshwa
tena katika nchi zao.
Pamoja na hayo amesema
kuna umuhimu wa kuwajengea uwezo wafanyabiashara na wajasiriamali wakubwa kwa
wadogo katika michakato yao yote ya utengenezaji bidhaa kuhakikisha suala la
viwango vya ubora haliachwi nyuma. Njia nyingine itakayosaidia wazalishaji wa
bidhaa kushindana na wenzao wa Afrika na kimataifa ni kuwaondolea vikwazo
mbalimbali ikiwemo kodi na masharti magumu ya kusafirisha bidhaa kutoka nchi
moja kwenda nyingine.
Frank Dafa, Meneja
Sera za Viwango wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) amesema katika
jumuiya hiyo wanaendelea kuondoa vikwazo vinavyowarudisha nyuma wafanyabiashara
na kuwafungulia fursa za kufaidika na masoko ya bidhaa ya kimataifa.
“Afrika Mashariki tumekuwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa kuweka mifumo ya kuoanisha sheria zetu za bidhaa ili kuhakikisha haziwi kikwazo kwenye biashara,” amesema Dafa.