Nchi za Afrika zatakiwa kuendeleza ushirikiano wa kibiashara ili kukuza uchumi.

Business / 8th November, 2022

Na Rajabu Msangi

 

Tanzania na Zimbabwe zimeendelea kushirikiana katika masuala ya kibiashara yakilenga kuongeza ushirikiano, kukuza diplomasia na kukuza uchumi baina ya mataifa hayo mawili.

 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara WIzara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bw. Christopher Mramba katika Mkutano wa uwekezaji kati ya Zimbabwe na Tanzania ambao umefanyika katika ukumbi wa Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.

 

“Kwa vile tumeshirikiana kwenye masuala ya kupigania uhuru wa kisisasa, sasa tunataka kuongeza mashirikiano kwa kukuza na kufikia uhuru wa kiuchumi na kibiashara” Amesema Bw. Mramba.

 

Aidha amesema kuna umuhimu wa Nchi za Afrika kuendeleza kushirikiana wenyewe kwa wenyewe katika biashara ili kuendeleza ukuaji wa uchumi baina ya nchi za Afrika na kukuza uwekezaji.

 

“Nchi za Afrika zinahitaji kufanya jitihada kubwa za kukuza biashara kati ya nchi za Afrika na nchi za Afrika yaani (Intra Africa Trade), kwa maana ya kwamba tumeshaingia kwenye makubaliano mbalimbali ya kikanda kama jumuiya ya Afrika Mashariki, tuna Mkataba wa SADC, tuna mkataba sasa hivi wa ushirikiano wa bara la Afrika”

 

“Hii ni hatua ambayo itatusaidia kuimarisha uchumi wetu, kujenga ajira kwa wananachi wetu, na kuwa na uchumi endelevu, hivyo tumesisitiza umuhimu wa nchi zetu kufanya biashara na kuondoa vikwazo vya kibiashara kati ya nchi zetu, kukuza biashara za mpakani” Ameongeza Bw. Mramba

 

Kwa upande wake Meneja Maendeleo ya Mauzo ya Nje kutoka ZimTrade Tatenda Marume amesema mkutano huo umelenga ajenda ya kuendeleza mahusiano ya kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Zimbabwe katika hali ya ushindi.

 

“Kwa mataifa mawili makubwa Tanzania na Zimbabwe, hawa ni watu wa kawaida sana ambao tunahitaji kubadilishana na tunatumai ni mwanzo wa mchakato ambao tunatumai kuwa sehemu mbili za sekta yetu kibinafsi zinakwenda Pamoja katika hali ya ushindi katika masuala ya kibiashara” Amesema Bw. Marume.

 

Naye Mkurugenzi wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mwajuma Hamza amesema mkutano huo umekuwa ni fursa kwa wafanyabiashara katika kutafuta wawekezaji lakini pia namna ya kuweza kuuza bidhaa nchini Zimbabwe.

 

“Lakini pia wenzetu wa Zimbabwe watatembelea baadhi ya viwanda hapa nchini kuweza kujionea namna ambavyo Tanzania tunazalisha bidhaa zetu na waone namna ya kuweza kufanya kazi Pamoja.” Amesema Mwajuma.