“Sheria ya Kulinda wawekezaji iangaliwe upya” Rais Samia
DODOMA
Rais Samia Suluh Hassan, amemtaka mwanasheria mkuu wa serikali, kupitia upya sheria ya kulinda uwekezaji, kwani sheria iliyopo ya kutaka migogoro yote baina ya nchi na mwekezaji kutatuliwa ndani ya nchi, imekuwa ikipelekea nchi kukosa wawekezaji wakubwa.
“Kuna mashauri ambayo kweli
tunaweza kuyafanya hapa ndani, lakini kwa mwekezaji aliye serious hawezi
kukubali, ukimpa kipengele hiki cha sheria anakimbia” amesema Rais Samia.
“Uwekezaji lazima
ulindwe, nendeni mkalinde uchumi wa nchi yetu kihaki na kiuwadilifu, ili nchi
yetu ipokee wawekezaji wengi Zaidi, tukuze uchumi na maslahi yapatikane zaidi”.
Rais Samia ameyasema hayo,
wakati wa mkutano wa Chama cha Mawakili nchini, uliofanyika leo Septemba 29,
2022 katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma, wenye kauli
mbiu “Utekelezaji wa Majukumu, unaotekeleza sheria na nyenzo muhimu kwa maendeleo ya taifa”
Aidha, Samia amesema
kutokana na serikali kuifungua nchi kwa kiasi kikubwa, imepelekea ongezeko kubwa
la wawekezaji nchini, hivyo mawakili watarajie ongezeko kubwa la migogoro ya
kibiashara au inayokinzana na sheria za nchi, hivyo ili kuwe na uwekezaji mzuri
wenye kukuza uchumi wan chi, mawakili wametakiwa kuwa makini katika kusikiliza
na kutatua migogoro hiyo.
Katika hatua nyingine,
Rais Samia amewataka wanasheria wote kuhahikisha wanajisajili, ili waweze
kutambulika na serikali.
“Wale ambao bado
hawajajisajili wanapaswa kujisajili, vinginevyo baada ya muda kupita
hatutawatambua kama mawakili wa serikali, itabidi watafute sekta nje waingie au
sijui watafanya utaratibu gani na Mwanasheria mkuu wa serikali ili wajisajili”.
Rais Samia, ametoa wito
kwa Wanasheria na Mawakili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sheria hususani
zinazowagusa sana wananchi, na taratibu ya jinsi ya kupata haki zao, lengo
likiwa ni kupunguza mlundikano wa mashauri ambayo hayana ulazima wa kufikishwa
mahakamani kwa utatuzi.
Miongoni mwa
waliohudhuria mkutano huo ni Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbalo,
Naibu Mwanasheria Mkuu wa serikali, Dkt Evaristo Longopa, Jaji mkuu wa Mahakama
ya Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Elieza
Mbuki Jeleshi, na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule.