Swissport Tanzania PLC yatoa gawio la Bilioni 1.73 kwa wanahisa

Swissport Tanzania PLC yatoa gawio la Bilioni 1.73 kwa wanahisa

Business / 27th May, 2022

Kampuni ya Swissport Tanzania Plc imefanya mkutano mkuu wa 37 kwa mwaka 2021 kwa kukutana na wanahisa waliowekeza katika kampuni hiyo na kujadili ajenda kuu tatu ikiwemo kupitia mahesabu ya kampuni kwa mwaka 2021 pamoja na kupitisha gawio kwa wanahisa ambao walipitisha gawio la shilingi bilioni moja na milioni 73.


Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam Afisa Mtendaji Mkuu wa Swissport Tanzania Plc Mrisho Yassin amesema kuwa, katika mkutano huo wa 37 wamekutana na wanahisa na kupitia ajenda mbalimbali ikiwemo ya kuweka mikakati katika kipaumbele cha mwaka huu wa 2022 kwa kuendelea mbele na kuhakikisha uthabiti katika utoaji wa huduma bora na salama kwa wateja wao pamoja na kufuatilia mwenendo wa biashara ili kuyafikia malengo ya biashara kwa mwaka.


''Katika mkutano huu ajenda kuu ilikuwa ni kupitisha mahesabu ya kampuni kwa mwaka 2021 ambayo wanahisa wameyapitisha, pia kulikuwa na ajenda ya ya kutoa gawio kwa wanahisa na kwa pamoja wanahisa wamepitisha gawio la jumla ya shilingi Bilioni moja na milioni 73 ambapo kila mwanahisa atapata gawio la shilingi 29.8 kwa share anayomiliki...Pia kupitia mkutano huu tutapata wajumbe wa bodi wawili kutoka kwa wanahisa wa kitanzania ili kufikisha wajumbe watano ambao watatu wanatoka katika kampuni Mama ya Swissport.'' Amesema.


Mrisho amesema, kwa mwaka 2020 kampuni hiyo haikutoa gawio kutokana na hasara ya shilingi bilioni moja na laki tano waliyoipata kutokana na athari la janga la UVIKO-19 na kwa mwaka 2021 walipata faida ya shilingi bilioni mbili la laki moja na gawio hilo litaanza kuingia katika mifuko ya wanahisa Julai, 5 mwaka huu.


Aidha amesema kuwa, wataendelea kuweka mikakati itakayoiwezesha kampuni kupata faida na wanamatarajio makubwa katika kukuza uchumi wa kampuni hiyo ambayo kwa sasa hisa moja ya Swissport inauzwa kwa shilingi elfu moja.


Pia Mrisho amesema kuwa wamekuwa wakishiriki shughuli za kijamii kwa kulipa kodi pamoja na kutoa ajira kwa watanzania ambapo hadi sasa wametoa ajira takribani 700 na baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua Royal Tour tayari wameanza kupokea watalii wengi na kuwahudumia kupitia anga na wanategemea matokeo chanya zaidi katika kukuza uchumi wa kampuni na Taifa kwa ujumla.


Kwa upande wake Mjumbe wa bodi ya kampuni hiyo na Mbunge wa Vunjo Dkt. Charles Kimei amesema, biashara kwa mwaka huu imekuwa nzuri na baada ya Royal Tour iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan watalii wameanza kuja kwa wingi na Swissport imekuwa ikiwahudumia kwa kiwango cha juu na ubora.


Kimei amesema kwamba mahusiano mazuri yanayojengwa na Rais Samia na Nchi nyingi duniani yana tija kwa Taifa na yanaleta biashara nzuri.


''Kibiashara hali sasa ni nzuri katika kampuni ya Swissport ambayo hata wakati wa Covid-19 ilifanya kazi nzuri kwa upande wa Cargo na kuvunja rekodi hasa katika bidhaa za maua na mbogamboga ambazo ni fursa... watanzania tuzichangamkie kupitia Swissport.'' Amesema.


Amesema Uongozi wa Swissport Tanzania ukiongozwa na Mrisho Yassin umejitahidi katika kutekeleza majukumu licha ya kuwepo kwa ushindani mkubwa na makampuni mengine na wameendelea kushikilia soko la huduma za ndege kwa asilimia 90 kwa ndege zinazoingia Tanzania.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Swissport Tanzania Plc Dirk Gooverts akiendesha kikao cha 37 kilichowakutanisha na wanahisa na kujadili ajenda mbalimbali ikiwemo kuboresha huduma pamoja na kutoa gawio kwa wanahisa hao.


Afisa Mtendaji Mkuu wa Swissport Tanzania Plc Mrisho Yassin (kushoto,) akizungumza wakati na mkutano huo na kueleza kuwa, katika mkutano huo wa 37 wamekutana na wanahisa na kupitia ajenda mbalimbali ikiwemo ya kuweka mikakati katika kipaumbele cha mwaka huu wa 2022. Leo jijini Dar es Salaam.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Swissport Tanzania Plc na Mbunge wa Jimbo la Vunjo Dkt. Charles Kimei (Katikati,) akizungumza na baadhi ya wanahisa waliohudhuria mkutano huo leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi wa washiriki wakichangia mada.