Serikali yafafanua mradi wa ujenzi bandari ya Bagamoyo

Serikali yafafanua mradi wa ujenzi bandari ya Bagamoyo

Business / 6th May, 2022

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Ashatu Kijaji amesema katika kipindi cha mwaka 2021/2022 imefufua majadiliano ya mradi wa Bandari na Kanda Maalum ya Bagamoyo (BSEZ) uliosimama tangu mwaka 2018.

 

Dk Kijaji ameyasema hayo leo Ijumaa Mei 6, 2022 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2022/2023.

 

Amesema wizara yake inaratibu uendelezaji wa BSEZ unaolenga kuendana na ushindani wa biashara za usafiri wa majini, pamoja na kuunganisha shughuli nyingine za kiuchumi ikiwemo viwanda na utalii.

 

Amesema katika mwaka 2021/2022, wizara imefufua majadiliano na wawekezaji wa Kampuni ya China, Merchants Holdings (International) Co. Ltd (CMHI) na Oman Investment Authority (OIA) ambayo awali ilikuwa inaitwa Mfuko wa Uwekezaji wa Serikali ya Oman (SGRF).

 

Amesema majadiliano hayo yanahusu eneo dogo la Mradi wa BSEZ kwa kuendeleza eneo la hekta 3,087 kati ya hekta 9,887 ambapo unahusisha ujenzi wa Bandari (Sea 38 Port).

 

Pia inahusisha ujenzi wa Kituo cha Usafirishaji kwenye eneo la hekta 887 na uendelezaji wa Eneo Maalum la Viwanda kwenye eneo la hekta 2,200.

 

“Msingi wa marejeo ya majadiliano hayo ambayo yalisimama mwaka 2018 ni kuhakikisha Serikali inatekeleza maeneo ambayo ni wajibu wake kama vile ujenzi wa miundombinu wezeshi (barabara, reli, umeme, maji, gesi na mifumo ya mawasiliano) na lango la kuingilia bandarini kwa maslahi mapana ya Taifa,”amesema.

 

Amesema uwekezaji katika maeneo ya Mradi yatafanywa kwa kuvutia wabia wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) au kufanywa na mwekezaji binafsi.

 

Aidha, Dk Kijaji amesema wizara kupitia Shirika la Viwango Nchini (TBS) imezuia bidhaa zisizokidhi viwango kutoka nje ya nchi kuingia sokoni shehena 1,517 na limeteketeza bidhaa zisizo kidhi ubora zenye thamani ya Sh6.73 bilioni.

 

“Sehemu kubwa ya bidhaa zilizozuiwa na zilizoondolewa kutoka sokoni zilikuwa ni bidhaa za chakula na vipodozi. Hatua stahiki zimechukuliwa kwa mujibu wa Sheria ikiwemo kuelimisha umma na bidhaa husika kuharibiwa,”amesema.