Serikali kulipa deni la malimbikizo.

Serikali kulipa deni la malimbikizo.

Business / 13th April, 2022

Serikali inatakiwa kulipa Sh 4.79 bilioni za malimbikizo ya riba yaliyotokana na kuchelewesha malipo kwa wakandarasi katika miradi sita ya uchukuzi.

 

 Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kuhusu ukaguzi wa miradi ya maendeleo, iliyotolewa Machi mwaka huu, imebainisha hayo.

 

Kichere ameitaja miradi hiyo sita na riba wanazodai wakandarasi kwenye mabano ni Programu ya Usaidizi wa Sekta ya Uchukuzi (Sh 1.39 bilioni), Uwezeshaji Biashara na Uchukuzi Kusini mwa Afrika (Sh 511.7 milioni) na Arusha Holili (Sh 2.2 bilioni).

 

Mingine ni Programu ya Uboreshaji wa Miundombinu ya Usafirishaji Jijini Dar es Salaam (Sh 349.8 milioni) na Mradi wa Multinational Rumonge-Gitaza-Kibondo-Kasulu-Manyovu (Sh 329.08 milioni).

 

“Nilibaini kuwa madai ya tozo ya riba yalisababishwa na ucheleweshaji wa kupokea fedha za miradi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango kutokana na ufuatiliaji usioridhisha wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na ambayo inazuia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kumlipa Mkandarasi kwa wakati,” amesema.

 

Hata hivyo, madai hayo ni kwa mujibu wa kifungu namba 51.1 cha masharti ya mkataba (GCC), unaomtaka mwajiri kumlipa mkandarasi kiasi kilichothibitishwa na meneja wa mradi ndani ya siku 28 tangu tarehe ya kila cheti.

 

“Ikiwa mwajiri atafanya malipo kwa kuchelewa, mkandarasi atalipwa riba kwa malipo yaliyocheleweshwa,” kinaeleza kifungu hicho.

 

Kwa mujibu wa Kichere, kuchelewa kuwalipa wakandarasi kunaongeza gharama na kunazorotesha shughuli za miradi ya maendeleo.

 

Kupitia ripoti hiyo, CAG amependekeza TANROADS kubainisha kwa uwazi vikwazo vya utekelezaji ili kuharakisha mchakato wa malipo na mamlaka nyingine zinazohusika na kuharakisha malipo ya madai ya wakandarasi yanayosubiriwa.

 

Ameishauri Wizara ya Fedha na Mipango kurahisisha taratatibu za kuchakata malipo kuwezesha fedha za miradi kupatikana kwa wakati kulingana na bajeti ili madai ya wakandarasi yalipwe kwa wakati.