NMB kwa kushirikiana na Jubilee life wamezindua rasmi Bima kwa ajili ya watu wenye kipato cha kati

Business / 20th December, 2021

Benki ya NMB kwa kushirikiana na Jubilee life wamezindua rasmi mpango wa Bima kwa ajili ya watu wenye kipato cha kati na wafanyabiashara nchini. Akizungumza katika uzinduzi huo, Bwana Filbert Mponzi amesema “Bima tunayoizindua leo tumeiita kwa jina la Fanaka Plan. Kwa makubaliano haya leo, watanzania wote bila kujali ana akaunti na NMB au lah, wataanza kujiwekea bima za Maisha kwaajili ya kutimiza malengo wanayotamani kuyafikia kwa kuwekeza kupitia Fanaka Plan” 

 

Fanaka inawawezesha wateja kutunza kiasi kidogo cha fedha kwa utaratibu maalumu na kiwango cha pesa kinachotunzwa ndani ya kila muda mteja alioutaka kuweza kutimiza malengo yake maalumu.

 

Jubilee Life Insurance wameweka na kutoa utaratibu wa malipo ambayo mteja atatakiwa kulipia mpango wake kwa muda atakaouridhia kukamilisha lengo alilojiwekea mfano kujenga nyumba ya ndoto yake, gari la ndoto yake au kupata mtaji wa biashara ya ndoto yake. 

 

Muda anaojiwekea mteja unaruhusu uwekezaji wa kati ya miaka 5-10 au 10-20 kulingana na atakavyojiwekea malengo yake. Muda wa mteja kupokea akiba zake alizotunza utakapowadia, mteja atapokea faida ya kati ya asilimia 10% mpaka asilimia 20% ya uwekezaji alioufanya pamoja na bonasi za kila mwaka zilizolimbikizwa. 

 

Iwapo mteja atafariki ndani ya muda wa uwekezaji, familia yake italipwa mpaka 175 % ya kiasi kilichopangwa kuwekezwa kutegemea chanzo cha kifo hicho. 

Iwapo mteja atapata ulemavu wa muda au ulemavu wa kudumu, atalipwa mara mbili ya kiasi alichopanga kuwekeza na hatoendelea kulipa badala yake, Jubilee Life wataendelea kumlipia mpaka kufikia muda wa mpango wenyewe. Mpango huu wa uwekezaji kupitia Fanaka plan, unatoa malipo ya faida ya ziada kwa wateja ambao wana mpaka miaka 90. 

Bidhaa hii ya fanaka inamuwezesha mteja kuwa na uhakika na uwekezaji wake na pia kutimiza malengo yake anayotamani kuyafikia. Mpango wa uwekezaji wa Fanaka unawapa wateja utulivu wa akili na usalama wa fedha zao katika kipindi cha mpango aliojiwekea. 

 

Filbert Mponzi amesema “Soko la Tanzania lina ushindani mkubwa lakini kila wakati tunajitahidi kwenda hatua moja mbele kubuni bidhaa mpya inayoongeza thamani kwa wateja wetu”