Faida za Mfumo mpya maombi ya kuunganisha umeme majumbani - TANESCO " NICONNECT”

Faida za Mfumo mpya maombi ya kuunganisha umeme majumbani - TANESCO " NICONNECT”

Business / 26th May, 2022

Mfumo mpya wa maombi ya kuunganisha umeme wa majumbani kwa wateja wa Shirika la kusambaza umeme nchini, TANESCO, " NICONNECT” unaelezwa kuwa utaondoa mianya ya kugushi na ucheleweshwaji wa huduma.


Hayo yamesemwa Mei 24, 2022 na wakandarasii waliokuwa wakipatiwa mafunzo ya kufanikisha mfumo huo mpya katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Mwenyekiti wa mafundi hao mkoani hapa, Engetraud Mbemba amesema kuwa kwa kipindi hiki ambacho maombi ya kuunganishiwa umeme yanafanyika kwa kujaza fomu, ghushi ni nyingi kwa pande zote za TANESCO na mafundi.

"Kuna watu wanaweza kuwa wanatumia leseni au mihuri ya mafundi wengine wenye sifa na kwa TANESCO kuna watu wanatumia mafundi kupitia wao., kulikuwa na watu maalum wanapata hizo kazi na wengine hawapati" amesema Mbemba.

Ameongeza kuwa kupitia mfumo wa sasa zoezi la uunganishaji umeme linachelewa kwa sababu mbali mbali ikiwemo nyaraka za maombi kupotea au mtu mmoja katika mnyororo wa kazi hiyo kuamua kuchelewesha zoezi kwa sababu zake binafsi.

Amefafanua kuwa kuwepo kwa mfumo mpya wa kufanya maombi kupitia mtandao, kutaondoa watu kupenya au kutumia leseni na mihuri ya mafundi wengine.

Hivyo amesema mafunzo hayo yatawasaidia kujua jinsi ya kutumia mfumo huo mpya hatimaye kuharakisha utendaji.

Aidha ametoa wito kwa shirika na mafundi wa umeme mkoani hapa kupenda kujifunza mifumo mbali mbali inayoharakisha shughuli zao za kila siku.

Fundi wa umeme wa wakala wa ufundi wa umeme nchini, TEMESA, Shaned Mapunda amesema kuwa mfumo uliopo sasa unatoa fursa kwa mafundi wasio wa TEMESA kufanya kazi ya kuunganisha umeme katika majengo ya serikali kwa kushirikiana na TANESCO lakini kupitia mfumo mpya hayo hayatawezekana.

" TEMESA ndio mhusika wa kufanya maombi ya kuunganisha umeme kwenye majengo ya serikali lakini shughuli hizi unakuta zinafanywa na mafundi wasio wa kwetu na TANESCO wanapitisha, naona haya mafunzo ni kitu kizuri kitapelekea kazi zetu kuwa rahisi" amesema Mapunda

Afisa teknolojia ya habari na mawasiliano, (TEHAMA) wa TANESCO Mtwara, Athumani Kunambi amesema kuwa mfumo huo mpya utamuwezesha mteja kujaza fomu ya maombi ya umeme popote alipo kwa kutumia simu au kompyuta yake na utaondoa urasimu na usumbufu kwa wateja au wakati mwengine kuchukuliwa pesa zao.


"Mfumo utapunguza muda kwa kiasi kikubwa na jinsi ulivyo mfumo unatutaka ndani ya siku nne kama kila kitu kitakua sawa basi mteja awe ameunganishiwa umeme" amesema afisa TEHAMA.

Afisa Uhusiano na huduma.kwa wateja wa TANESCO mkoani hapa, Jumanne Nkhungu amesema kuwa mafunzo hayo yamedhamiria kuwapatia taarifa na maarifa mapya ya mfumo wa *niconnect wakandarasi wa kutandaza umeme majumbani kutoka Manispaa ya Mtwara Mikindani wapatao 13.

Amesema watafanya hivyo kwa wakandarasi wa mkoa mzima ili mfumo utakapoanza wawe na ujuzi nao.

"Hakika mfumo utapunguza muda wa zoezi la kuomba kuunganishiwa umeme, kwa sasa mteja analazimika kuja kwetu mara tatu, kufanya maombi, kurudisha fomu ya maombi kisha kuja kuchukua namba ya malipo" amesema Nkungu.

Kwa sasa mfumo huo mpya tayari umeanza kutumika katika mikoa ya Dar es salaam na Pwani na unaelezwa kuonyesha ufanisi.