Equity Bank Group kuwekeza Trilioni 13

Equity Bank Group kuwekeza Trilioni 13

Business / 9th June, 2022


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru (kulia), akizungumza na Afisa Mipango Mkuu wa Equity Bank Group Bw. Brent Malay, Ofisini kwake Jijini Dodoma ambapo Benki hiyo inataka kuongeza uwekezaji wake nchini Tanzania.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru, akifafanua jambo alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Equity Bank Group (haupo pichani) ofisini kwake-Treasury Square-Dodoma, ambapo Benki hiyo inataka kuongeza uwekezaji wake katika sekta mbalimbali kwa njia ya kutoa mikopo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity-Tanzania, Bi. Isabela Maganga, akiekeza kuhusu mikakati ya Benki hiyo kuwekeza sh. trilioni 13 katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania ili kuendeleza sekta mbalimbali kwa njia ya utoaji mikopo, ofisini kwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru, Jijini Dodoma. Kushoto ni Afisa Mipango Mkuu wa Equity Bank Group Bw. Brent Malay.

Kamishna Idara ya Usimamizi wa Deni la Taifa Bw. Japhet Justine (kushoto), Mkuu wa Malipo wa Equity Bank Tanzania Bw. Ralph Ligallama (kulia), wakifuatilia mjadala kuhusu kusudio la Benki hiyo kuongeza uwekezaji wa rasilimali fedha kwenye miradi ya kimkakati katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ofisini kwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru, Jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru, ameihakikishia Benki ya Equity Group kwamba Serikali iko tayari kushirikiana na Benki hiyo kutekeleza Mpango Mkakati utakaowezesha upatikanaji wa zaidi ya shilingi trilioni 13 zilizopangwa kutolewa na Benki hiyo kuendeleza mipango mbalimbali ya maendeleo kikiwemo kilimo katika nchi za Afrika Mashariki.

Bw. Mafuru amesema hayo jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Benki hiyo yenye makao yake Makuu nchini Kenya.

Alisema kuwa Benki hiyo imedhamiria kuwekeza fedha katika maeneo sita ikiwemo sekta za kilimo, madini, uendelezaji wajasiliamali wadogo na wa kati, mazingira, utawala bora, viwanda na sekta ya biashara.

Bw. Mafuru alisema kuwa maeneo hayo ya miradi ya kimkakati yanakwenda sambamba na na ukuzaji wa mipango ya kitaifa ikiwemo sekta ya kilimo ili sekta hiyo iwe na tija zaidi kwa kuongeza uzalishaji wa mazao na kuyaongezea thamani.

“Equity Bank Group wanataka kuwekeza hapa nchini katika maeneo mbalimbali kikiwemo  kilimo kwa kuongeza mifumo ya umwagiliaji na kuimarisha utunzaji na kuzuia upotevu wa mazao wakati na baada ya mavuno” alisema Bw. Mafuru.

Alisema kuwa Benki hiyo pia imekusudia kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kwa kuyachakata hapa hapa nchini kabla ya kuyapeleka kuuzwa ndani na nje ya nchi hatua itakayoongeza mnyororo wa thamani, ubora wa bidhaa ili kushindana katika soko.

Bw. Mafuru alifafanua kuwa uwekezaji huo utagusa maeneo mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo kukuza ajira na kuviwezesha viwanda vilivyoko katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kupata malighafi na soko la uhakika hususan baada ya nchi ya DRC Kongo kujiunga na Jumuiya hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Ujumbe wa Benki hiyo ulioongozwa na Afisa Mipango Mkuu Bw. Brent Malay, Mkurugenzi Mtendaji wa Equity Bank Tanzania, Bi. Isabela Maganga, alisema kuwa Benki yao inataka kushirikiana na Serikali kukuza uchumi wa nchi na kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Alieleza kuwa uwekezaji wa kiasi cha shilingi trilioni 13 unaotaka kufanywa na Benki hiyo katika Nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania, utakuwa wa kipindi cha miaka mitano ambapo watatoa mikopo kwa watu milioni 5 na kuzalisha ajira milioni 50.

Bi. Maganga alieleza kuwa Benki ya Equity inataka kuongeza uwekezaji wake hapa nchini ili kuchochea uzalishaji katika maeneo ya kipaumbele na kuhakikisha kuwa watanzania wengi wanafikiwa na mpango huo ili wajikwamue kiuchumi.