Dkt. Biteko awataka wachimbaji madini kushirikiana na vyombo vya ulinzi kubaini watoroshaji madini

Dkt. Biteko awataka wachimbaji madini kushirikiana na vyombo vya ulinzi kubaini watoroshaji madini

Business / 30th May, 2022

Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema licha ya kuwepo kwa jitihada za Vyombo vya Ulinzi na Usalama, uanzishwaji wa masoko na kufutwa kwa tozo mbalimbali lakini bado kuna baadhi ya watu wasio waaminifu wanatorosha madini.

Dkt. Biteko ameyasema hayo wakati akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika eneo la Lwamgasa mkoani Geita ambapo amewataka waachane na tabia ya kutorosha madini na badala yake wayapeleke sokoni.

Aidha, Dkt. Biteko amewataka wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu pamoja na watanzania wote kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama ili kuwabainisha watoroshaji wa madini nchini.

Dkt. Biteko amesema madini ya dhahabu yanayotokana na Mialo hayaonekani sokoni ambapo amesema kuna uwezekano mkubwa kwamba dhahabu inayo chenjuliwa kwenye Mialo inatoroshwa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatamani kuona watanzania wanabadili maisha yao kupitia Sekta ya Madini.

“Saa ya nyinyi kufanya kazi na kutajirika ni sasa, Mama yetu Mhe. Samia Suluhu Hassan anatamani kutuona wachimbaji wadogo wa madini tunatajirika na tunabadilisha maisha yetu kupitia uchimbaji wa madini,” amesema Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita Rosemary Senyamule amesema Mkoa wake anajipanga kuandaa mazingira yatakayopelekea kuujenga mkoa huo kuwa kitovu cha madini ya dhahabu Afrika ambapo mikoa mingine na nchi za jirani watajifunza kupitia mkoa huo.

“Tunatamani Mkoa wetu wa Geita kuwa kitovu cha madini ya dhahabu sio tu kwa Tanzania bali Afrika kwa ujumla,” amesema Senyamule.

Pia, Senyamule amesema mkoa wa Geita umeanza kujenga majengo ya kudumu kwa ajili ya Maonyesho ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta Madini ili yawe na hadhi ya kimataifa.