Brela kufuta kampuni 5,676

Brela kufuta kampuni 5,676

Business / 27th May, 2022

Makampuni 5,676 ambayo ni awamu ya kwanza yanayotarajiwa kufutwa kwani Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) inabidi hayafanyi biashara kwa kutotimiza matakwa ya kisheria kama nilivyoeleza hapo juu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa amesema kuwatangu uteuzi wake mojawapo ya changamoto aliyokutana nayo ni uwepo wa makampuni mengi ambayo hayafanyi kazi au shughuli yoyote ya kibiashara katika Daftari la Makampuni.

Pia amesema kuwa yapo Makampuni yenye miaka zaidi ya 50 na hayana uthibitisho kuwa yanafanya biashara na hayawasilishi Taarifa za Mwaka (Annual Return) kwa kampuni zilizosajiliwa hapa nchini au Mizania ya Mwaka (Financial Statements) kwa kampuni zilizosajiliwa nje ya nchi.

"Kifungu cha 128 cha Sheria ya Makampuni, Sura 212 kinazitaka Kampuni zilizosajiliwa hapa nchini kuwasilisha Taarifa za mwaka “Annual Return” ambapo kutofanya hivyo kunatupa tafsiri kuwa huenda kampuni hii haifanyi biashara kulingana na lengo la uanzishwaji wake." Alisema Nyaisa

Na pia Nyaisa amesema Kifungu cha 438 cha sheria ya Makampuni kinazitaka Kampuni zilizosajiliwa nje ya nchi ambazo zina Ofisi za Biashara nchini kuwasilisha Mizania ya Mwaka (Financial Statement) ambapo kutofanya hivyo pia kunatoa tafsiri kuwa kampuni hizo hazifanyi biashara hapa nchini.

"Vifungu vya 400 na 441 vya Sheria ya Makampuni vinanipa mamlaka mimi kama Msajili wa Makampuni kufuta makampuni ambayo hayafanyi biashara. Uwepo wa makampuni mengi yasiyofanya biashara ni kinyume na sheria na ni mzigo kwa Wakala kwa kutunza kumbukumbu za Makampuni mengi ambayo hayafanyi biashara au yameshikilia majina kinyume cha sheria kwa ajili ya kuwauzia watu wengine wenye uhitaji wa majina hayo." Alisema Nyaisa

Nyaisa amesema ameamua kutumia vifungu tajwa hapo juu vya Sheria kuanzisha mchakato wa kufuta kampuni ambazo hazifanyi biashara na haziwasilishi Taarifa za Mwaka na Mizania ya Mwaka katika Daftari la Makampuni. Zoezi ni endelevu na litafanyika kwa awamu hadi pale tutakapojiridhisha kuwa kampuni zilizopo kwenye Daftari ni zile zinazofanya biashara.

"Endapo kampuni yako itakuwa imefutwa ina maana kama kampuni ilikuwa na mali basi mali hizo zitakuwa zimepotea, au wamiliki wa kampuni watalazimika kwenda mahakamani kuomba mahakama kuirejesha kampuni hii kwenye Daftari la Makampuni “Company restoration” kwa mujibu wa sheria." Alisema Nyaisa

Pia ametoa rai kwa Kampuni zilizosajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni, Sura 212 ambazo hazijaorodheshwa kwenye Orodha ya awamu ya kwanza, kutekeleza matakwa ya Sheria hiyo ili kuepuka kufutwa kwenye Daftari la Makampuni kwani zoezi hili ni endelevu. Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Makampuni 5,676 ambayo ni awamu ya kwanza yanayotarajiwa kufutwa usajili wa BRELA, mkutano huu ulifanyika makao makuu ya Wakala hiyo yaliyopo jijini Dar es Salaam.


Kaimu Mkurugenzi wa Makampuni na Majina ya Biashara wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Meinrad Rweyemamu(wapili Kulia) atolea ufafanuzi baadhi ya maswali yaliyokuwa yanaulizwa na waandishi wa habari kwenye mkutano huo uliofanyika katika makao makuu ya ofisi hizo jijini Dar es Salaam.