Bilioni 500 kutumika kuimarisha upatikanaji umeme nchini

Bilioni 500 kutumika kuimarisha upatikanaji umeme nchini

Business / 20th May, 2022

SERIKALI  imetenga jumla ya shilingi bilioni 500 zimepangwa kutumika kuimarisha upatikani wa umeme wa uhakika nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nishati January Makamba alipokuwa akiwasilisha taarifa ya Wizara ya Nishati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wakati wa mkutano na wananchi wa mkoa wa Tabora kwenye uwanja Ali Hassan Mwinyi kufuatia ziara Rais mkoani humo.

Waziri Makamba ameeleza kuwa, Bilioni 25 zitatumika kwaajili ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kwenye kituo cha Uhuru ambacho kitaboresha upatikanaji wa umeme kwenye wilaya za Urambo, Kaliua.

Akizungumzia kuhusu changamoto ya upatikanaji wa umeme nchini na katika wilaya za urambo na Kaliua, Waziri Makamba amebainisha kuwa, tunapozungumzia upatikanaji wa umeme wa uhakika, tunazungumzia waya zenye urefu na unene sahihi, tunaongelea transforma zenye ukubwa sahihi, tunazungumzia vituo vya kupokea na kupoza umeme vyenye kutosheleza mahitaji.

Amesema kuwa, kukiri changamoto sio udhaifu bali ni nyenzo ya kujiimarisha.

“ukweli ni kwamba tumepata changamoto kubwa ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kutokana na kwamba hatukufanya uwekezaji unaoendana na wakati na Mahitaji. Kwamba kwa miaka mingi hatukufanya uwekezaji kwenye uzalishaji na miundo mbinu unaoendana na wakati lakini na mahitaji ya kutosheleza.” Amesema Waziri Makamba.

Waziri Makamba ameeleza zaidi kuwa, matokeo yake ni kwamba mfumo wa gridi nzima ya Taifa, umeelemewa kutokana na kuongezeka kwa mahitaji lakini pia kutokana na uchakavu.

Amesema, Katika wilaya ya Urambo na Kaliua kumekuwa na changamoto ya kukatika kwa umeme kutokana na njia za umeme zinazopelekea umeme katika wilaya hizo kuwa zimetembea umbali mrefu yakribani umbali wa kilometa 1200 na hivyo kusababisha kuwepo kwa hitilafu ya umeme katika maeneo hayo kwa vile umeme unasambazwa kwa umbali mrefu na hivyo nguvu ya umeme inapungua.

Aidha, kutokana na mahitaji ya umeme kwenye wilaya hizo kipindi hicho yalikuwa madogo, nyaya zilizotumika zilikuwa ndogo za mm25 baada ya mahitaji kuongezeka waya hizo zikawa hazikidhi mahitaji.

Waziri Makamba amesema, Ili kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme wa uhakika katika wilaya za Urambo na Kaliua Mkoani Tabora, Wizara ya Nishati kupitia shirika lake la TANESCO, limechukua hatua ya dharura kwa kutoa milioni 509 ambazo zilitumika kufanya ukarabati kwa kubadilisha nyaya kutoa nyaya ndogo za mm 25 na kuweka nyaya  za mm 100 kwa umbali wa km 53 na kazi hiyo imeshakamilika.

Amesema, kazi nyingine za kubadilisha vikombe chakavu zinaendelea.

Waziri Makamba amesema, tayari utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vituo vya kupokea na kusambaza umeme vya Uhuru Wilayani Urambo na Ipole Wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora umeanza.

Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 25 ambapo, bilioni 5 zitatumika kwa ajili ya ulipaji wa fidia na bilioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa njia za kusafirisha umeme na ufungaji wa mitambo katika vituo vya Uhuru na Ipole.

Amesema, kukamilika kwa mradi huu kutasaidia kuiunganisha mikoa ya Kigoma na Katavi na Umeme wa Gridi ya Taifa hivyo, mikoa hiyo kuondokana na umeme wa jenereta ambao umekuwa ukiigharimu Serikali kiasi kikubwa cha fedha.

Waziri Makamba aliongeza kuwa, Shirika la TANESCO linahitaji maboresho makubwa ili kuimarisha huduma ya upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.

Akizungumzia kuhusu Utekelezaji wa Miradi ya umeme Vijijini (REA) kwa Mkoa wa Tabora, Waziri Makamba amesema vijiji vyote vilivyobakia ambavyo bado havijaunganishiwa umeme vitapatiwa umeme kama ilivyopangwa.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu Mhe. Rehema Migila alilalamikia kuhusu kukatika kwa umeme katika jimbo lake na Mbunge wa jimbo la Urambo Mhe. Magreth Sitta pia alielezea changamoto hiyo hiyo ya kukatika kwa umeme jimboni kwake na kusema kuwa anaamini Waziri wa Nishati atalipatia ufumbuzi tatizo hilo.