Barrick Bulyanhulu yaendelea kufanya uwekezaji katika huduma za kijamii, yatenga Bilioni 1.9 mwaka 2022

Barrick Bulyanhulu yaendelea kufanya uwekezaji katika huduma za kijamii, yatenga Bilioni 1.9 mwaka 2022

Business / 6th June, 2022


Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, umesaini mkataba wa makubaliano na Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC)  Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga ambapo umetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya kufanikisha miradi mbalimbali ya kijamii kupitia bajeti ya fedha zilizotengwa kufanikisha miradi ya kusaidia jamii (CSR) katika kipindi cha mwaka 2022.
 
 
Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo imefanyika katika mgodi wa Bulyanhulu na kuhudhuriwa na viongozi wa mgodi wa Bulyanhulu na watendaji kutoka Halmashauri ya wilaya ya Msalala na wafanyakazi wa mgodi huo.
 
Akiongea katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala, Mhe. Mibako Mabubu, aliipongeza Barrick Bulyanhulu kwa mchango mkubwa inaotoa kufanikisha jitihada za Serikali kuboresha huduma za kijamii na miundo mbinu katika wilaya hiyo.
 
 
Hivi karibuni Kampuni ya Barrick , ilitangaza kuwa itatumia dola 6 kwa kila wakia ya dhahabu inayouzwa na migodi yake miwili nchini katika kuboresha huduma za afya, elimu, miundombinu na upatikanaji wa maji safi ya kunywa katika jamii zinazowazunguka.
 
 
Wakati huo huo, imetoa hadi dola milioni 70 kwa ajili ya uwekezaji katika miradi ya kitaifa ya kuongeza thamani, ikijumuisha mafunzo yanayohusu madini, ukuzaji ujuzi na vifaa vya kisayansi katika vyuo vikuu vya Tanzania, pamoja na miundombinu ya barabara.
 
Hii ni kwa mujibu wa masharti ya msingi ya makubaliano ya mfumo wa Barrick na Serikali, ambayo yalihusishwa na kuanzishwa kwa ubia wa pamoja na Twiga. Twiga inasimamia mgawanyo wa 50/50 wa faida za kiuchumi zitokanazo na migodi pamoja na uongozi wake.
 
Rais wa Barrick na Afisa Mtendaji Mkuu Mark Bristow, alisema mpango wa uwekezaji ulikuwa mageuzi ya hivi karibuni ya ushirikiano wenye mafanikio makubwa baina ya kampuni na Serikali.
 
 
Barrick, imetumia zaidi ya dola bilioni 1.9 katika kodi, mishahara na malipo kwa wafanyabiashara wa ndani katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Angalau 73% ya bidhaa na huduma za migodi hiyo zinapatikana ndani ya nchi na inatoa kipaumbele kwa kuajiri wazawa wa Tanzania.