Ufafanuzi Mabadiliko ya bei za bando watolewa

Ufafanuzi Mabadiliko ya bei za bando watolewa

General / 21st November, 2022

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe.Nape Nnauye amesema hakutakuwa na mabadiliko ya bei za bando hadi tathmini ya gharama itakapokamilika ambapo tathimini inayofanywa kila baada ya miaka mitano, inatarajiwa kukamilika kati ya Desemba 2022 hadi Januari 2023. 


Mhe. Nape ametoa kauli hiyo leo Novemba 21, 2022 wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), jijini Dar es Salaam akisema kwa sasa watoa huduma wote wako katika viwango vya bei elekezi iliyowekwa na Serikali ambayo ni kati ya Sh2.03 hadi Sh9.35. 


"Hatutegemei mabadiliko yoyote kwa kipindi hiki hadi tathmini itakapokamilika, niwaombe wananchi wasione hatuhangaiki na suala hili, tumekuwa tukihangaika nalo." 


"Sasa tumefikia hatua ambayo tumesema tutatulia hadi tathmini itakapokamilika na matumaini yetu kuwa itatupa muelekeo mzuri," amesema Nnauye