BENKI YA DUNIA YAPONGEZWA KWA MAFUNZO YA REGROW

BENKI YA DUNIA YAPONGEZWA KWA MAFUNZO YA REGROW

General / 14th March, 2024
Wataalam kutoka Benki ya Dunia wamepongezwa kwa kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa na wataalam wanaotekeleza Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) wa kushughulikia malalamiko (GRM) na maoni yanayolenga utekelezaji wa mradi. 

Akifunga Mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa hao, Mkaguzi Mkuu wa Ndani Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Anakretus Mhidze amesema mchango huo wa Benki ya Dunia kwa njia ya Mafunzo kwa Wataalam hao, ni wathamani kubwa kwa kuwa unakwenda kuboresha zoezi zima la upokeaji wa malalamiko kupitia mfumo maalum wa Mradi wa REGROW.

Bw . Mhidze ameongeza kuwa mradi wa REGROW unaendelea kuleta matokeo chanya na kuwa msaada mkubwa kwa wananchi huku ukitarajiwa kuimarisha zaidi uhifadhi na Utalii Kusini mwa Tanzania hivyo uwepo wa mafunzo hayo ni hatua muhimu kupelekea kufikia malengo ya mradi huo.Aidha Bw. Mhidze amewaeleza wahitimu wa mafunzo hayo kuwa Mafunzo waliyopata ni ya muhimu sana kwani yatawasaidia kutekeleza Mfumo wa kushughulikia malalamiko bila kikwazo na kuhakikisha malalamiko yoyote yanayotokana na utekelezaji wa shughuli za mradi yanapokelewa na kushughulikiwa kwa wakati.

"Kupitia mafunzo haya ninyi mmekuwa wahitimu na mabalozi mnaoweza kuwafundisha wengine utekelezaji wa mfumo huu kwa kushirikiana nao katika kupokea na kushughulikia malalamiko yanayohusu mradi" alisisitiza Bw. Mhidze 

Kwa mujibu wa msimamizi wa Mafunzo wa mradi Bw. Loramatu Meikoki, Mafunzo hayo yameshirikisha Wataalam kutoka Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Tume ya Taifa ya  Umwagiliaji (NIRC), Bodi ya Maji ya Mto Rufiji  (RBWB), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) na Wizara ya Maliasili na Utalii (MNRT).