Wizara ya Ardhi yaanika Mafanikio utekelezaji wa Masuala ya Sekta ya Ardhi Nchini

General / 3rd January, 2023

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula amesema Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ameridhia ardhi yenye ukubwa wa ekari 1,492,703 iliyokuwa sehemu ya maeneo ya hifadhi na maeneo ya umma zikiwemo Ranchi za Serikali kumegwa na kurasimishwa kwa wananchi.

Ameyasema hayo leo Januari 03, 2023 wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusumasuala mbalimbali ya sekta ya ardhi na muelekeo wa utekezaji wa Wizara hiyo kwa kipindi cha kuanzia  januari 2023.

“Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta imeielekeza Mikoa kusimamia utekelezaji wa uamuzi wa Serikali kwenye maeneo yao yote yalioainishwa na kutolewa uamuzi” amesema Dkt. Mabula. 

Dkt.Mabula, amesema mongoni mwa kazi zinazondelea kutekelezwa hivi sasa ni pamoja na uwekaji wa alama za mipaka baina ya maeneo ya hifadhi na maeneo ambayo Serikali imeridhia yabaki kwa wananchi, upangaji na upimaji wa maeneo yaliyorejeshwa kwa wananchi, utambuzi, uhakiki na uthamini wa maeneo ambayo wananchi watatakiwa kupisha shughuli au maeneo yatakayotumika kwa matumizi ya umma na uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi.


Aidha, Mapori Tengefu 12 yenye ukubwa ekari 707,962 na Hifadhi za Misitu Misitu 7 zenye ekari 46,715 nayo imefutwa na ardhi hiyo kukabidhiwa kwa wananchi kupitia usimamizi wa Serikali za Mikoa katika kupanga na kuyapima maeneo hayo.

Kuhusu suala la ulipaji kodi ya pango la ardhi hasa baada ya msamaha wa riba ya malimbikizo ya pango la ardhi uliotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ambapo wananchi wenye malimbikizo walipewa nafuu ya kulipa deni la msingi ili wasamehewe riba ya malimbikizo.  Waziri wa Ardhi alieleza kuwa, Kutokana na nafuu uliotolewa  Wizara yake imeweza kukusanya jumla ya shs 90,907,939,421 sawa na asilimia 75 ya lengo la nusu mwaka. 


Hadi kufikia Novemba, 2022 wananchi 2,819 wamenufaika na msamaha wa riba ya malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi yenye jumla ya TZS 6,946,930,272. Idadi hiyo haijumuishi wananchi waliojitokeza ambao wamehudumiwa kuanzia tarehe 1 – 31 hadi Disemba 31, 2022. 

Amewashukuru na kuwapongeza wamiliki wa ardhi waliojitokeza kunufaika na msamaha uliotolewa na Mhe. Rais na kubainisha kuwa, katika mwezi Disemba, 2022 Wizara ya Ardhi imeshuhudia idadi kubwa ya wamiliki waliojitokeza kulipa na kiasi cha bilioni 22.6 kimekusanywa katika mwezi Disemba pekee. 

Katika hatua nyingine Dkt. Mabula amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia kikamilifu mipango ya jumla, mipango kina na mipango ya matumizi ya ardhi vijijini kupitia kamati za ardhi za Vijiji ili kudhibiti ujenzi holela usiozingatia mipango iliyoandaliwa na kuidhinishwa kupitia Kamati za Mipangomiji. 

“wizara imekuwa ikipokea taarifa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu ukiukwaji wa taratibu mbalimbali zinazohusu Usimamizi wa Ardhi Mijini na Vijijini” alisema Dkt Mabula

Miongoni mwa malalamiko ni baadhi viongozi wa vijiji na Mitaa kuuza ardhi kinyume na utaratibu, kukosekana kwa udhibiti wa uendelezaji ardhi katika maeneo ya Vijiji na Miji. Hali hiyo imesabisha kuongezeka kwa migogoro ya ardhi na uendelezaji ardhi kinyume na mipango iliyoandaliwa na kuidhinishwa.

Dkt Mabula amesema Wizara yake inaandaa programu maalum ya kufanya ukaguzi wa uzingatiaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kwa Mamlaka za Upangaji. Taarifa hizi zitatolewa kwa umma kama sehemu ya uwajibikaji wa mamlaka zetu kwa wananchi.

Kuhusu ujenzi wa vituo vya mafuta, Dkt. Mabuka alisema hadi kufikia tarehe 31 Disemba, 2022 Wizara imepokea taarifa ya uendelezaji wa vituo vya mafuta kutoka Halmashauri 129 kati ya 184 zilizopo nchini sawa na asilimia 70.1.

Uchambuzi uliofanywa na Wizara ya Ardhi umebaini katika Halmashauri 129, kuna vituo 2,063 ambapo kati ya hivyo vituo vya mafuta ni 1269 (asilimia 61.6) na vituo vidogo vya mafuta ni 794 (asimilia 38.5) huku Vituo 1,868 vimejengwa katika umbali wa zaidi ya mita 200 kutoka kituo kimoja na kingine sawa na asilimia 90.5 kama inavyoelekezwa na kanuni ya viwango vya umbali

Aidha,  Vituo 195 vimejengwa umbali wa chini ya mita 200 sawa na asilimia 9.5. Wizara inaendelea kufanya uchambuzi zaidi ili kubainisha vituo ambavyo vimejengwa kabla au baada ya kanuni za mwaka 2018 zinazoendelea kutumika ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa.