NMB kukuza Vipaji vya Ubunifu, Mageuzi ya Kidijitali UDSM Co-ICT

NMB kukuza Vipaji vya Ubunifu, Mageuzi ya Kidijitali UDSM Co-ICT

General / 24th October, 2024

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

BENKI ya NMB na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wamesaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano, unaolenga kukuza vipaji, ubunifu, uwekezaji katika mageuzi ya kidigitali na msaada wa kifedha kwa wanafunzi wa Chuo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Co-ICT), kilicho chini ya chuo hicho.

Makubaliano hayo ya miaka mitano, yamesainiwa leo Jumatano Oktoba 23 Makao Makuu ya NMB jijini Dar es Salaam huku UDSM ikiwakilishwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Utafiti, Profesa Nelson Boniface wakati NMB imewakilishwa Afisa Mkuu wa Rasirimali Watu, Emmanuel Akonaay.

Akizungumza kabla ya kusaini mkataba huo, Akonaay alisema NMB ambayo elimu ni sekta ya kipaumbele, inaamini kuwa makubaliano hayo yanaenda kuchochea ubunifu miongoni mwa wanafunzi wa Co-ICT, ambao utawezesha utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoizunguka jamii na taifa kwa ujumla.

Alibainisha ya kwamba makubaliano hayo yatajikita katika maeneo matano ya; Ukuzaji Vipaji na Ujuzi, Ukuzaji Ubunifu wa Matumizi ya Teknolojia, Uwekezaji katika Mageuzi ya Kidigitali, Utafiti Teknolojia na Maarifa, pamoja na Msaada wa Kifedha wa Masomo kusaidia programu bunifu.

“Katika Ukuzaji wa Vipaji na Ujuzi, kwa pamoja NMB na Co-ICT tutashirikiana katika kutambua na kuendeleza kupitia mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika Nyanja za TEHAMA, kama itakavyokuwa kwenye Ukuzaji wa Ubunifu wa Matumizi ya Teknolojia.

“Hapo tutasaidia kuendeleza ushindani katika Sekta ya Fedha ambayo inakua kwa kasi sana, pande zote zitashirikiana katika kutoa fursa kwa wanafunzi kujaribu teknolojia tofauti zinazoweza kuwa na athari chanya kwa sekta ya kifedha kupitia SANDBOX,” alifafanua Akonaay.

Aliongeza ya kwamba, katika Mageuzi ya Kidigitali, NMB na Co-ICT kwa pamoja watawekeza kwenye nyanja hiyo ili kuongeza ufanisi, kupunguza gharama na kuboresha huduma kwa wateja na katika Utafiti wa Teknolojia na Maarifa, watashirikiana kufanya utafiti wa kiteknolojia ili kuchunguza athari zake kwa Sekta ya Fedha.

“NMB tunaamini makubaliano haya sio tu yatasiadia kuimarisha mahusiano yetu, bali ni muendelezo wa mashirikiano endelevu baina yetu na ahadi yetu ni kuwa NMB itaendelea kufanya kazi na Serikali yetu katika Sekta ya Elimu, ambayo ni utekelezaji wa dhati wa dhamira yetu ya kuchangia ukuaji na ustawi wa elimu nchini.

“Tunaishukuru UDSM Co-ICT kwa kuichagua NMB na kukubaliana kushirikiana katika kufanikisha matakwa ya kimkataba,” alisema Akonaay aliyemwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna ambaye alishindwa kuhudhuria hafla hiyo kutokana na mkwamo wa kimajukumu.

Ukiondoa makubaliano hayo, mchango na mashirikiano mengine baina ya NMB na UDSM ni mkataba wa miaka miwili na Shule Kuu ya Biashara ya UDSM, ambako kwa miaka miwili imetumia Sh. Mil. 35 kwa ajili ya kuwazawadia wanafunzi watatu bora waliofanya vizuri zaidi katika Masomo ya Biashara.

“Pia, NMB tumekuwa tukiandaa Career Fairs, ambayo tumeyatumia kuwakutanisha mamia ya wanafunzi, sio tu kuwaonesha aina ya huduma zetu, bali kuwafunza namna ya kuomba kazi na kuwajengea uelewa wanafunzi wanaojiandaa kuingia katika soko la ajira, kuwajuza changamoto na mahitaji ya soko.

“Lakini pia, kupitia NMB Foundation, tumekuwa tukitoa ufadhili wa NMB Nuru Yangu Scholarship and Mentorship, ambapo hadi sasa tunq wanafunzi 132 wako katika vyuo mbalimbali vya umma, ambako wametengewa kiasi cha Sh. Bilioni 1.4 ili kuwawezesha kupata masomo yao hasa watokao mazingira magumu,” alisema.

Aidha, Akonaay alisema benki yake imekuwa pia ikitoa programu ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi, ambapo jumla ya wanafunzi 1,500 waliomaliza vyuo vikuu wamekuwa wakifanya mafunzo hayo, wengi wao wakiwa wamechukuliwa na NMB na wengine wameajiriwa kwingineko.

Kwa upande wake, Profesa Nelson aliishukuru NMB kwa kukubali kuingia mkataba wa makubaliano hayo, yanayompa uhakika kwamba yanaenda kuwawezesha vijana wazuri wa ubunifu ambao watanufaika vya kutosha kupitia makubaliano hayo, yanayoenda pia kuchachua teknolojia ya Akili Mnembaa ‘Artificial Intelgency’ (AI).

“Tulikupokuwa tunateta kwamba, AI itakuwa ni sehemu ya mambo ambayo yatatekelezwa kupitia makubaliano haya, lakini je AI tulizonazo zinajua kuongea lugha zetu tunapofanya biashara? Sasa hiyo ni ‘challenge’ ambayo tunapaswa ‘kui-address’ kwenye muundo wa kibiashara uliomo kwenye mkataba huu.

“Hii maana yake ni kuwa itatulazimu tutapowaendea watu wasiojua Kiingereza, wasiojua Kiswahili, tuweze kuwafikia kwa lugha zao za asili ili kufanikisha malengo na mipango ya kibiashara. Nadhani hapo NMB itakuwa ‘giants’ wa ubunifu,” alisema Profesa Nelson.

Alibainisha na kusisitiza kuwa UDSM na Co-ICT inao vijana wengi, wazuri na mahiri katika katika ubunifu, anaodhani wakati wao kunufaika na makubaliano hayo ni sasa na kuwataka NMB kusapoti harakati zao sio tui li kuwawezesha kuingia katika soko la ajira, bali kujiajiri itakapolazimika.

“Tunawashukuru sana NMB kwa namna wanavyoyafanyia kazi makubaliano tunayoingia baina yetu, kwa sababu hii sio mara ya kwanza kusaini mikataba ya aina hii, kama ilivyotanguliwa kusemwa na Bwana Akonaay, ambako wametupa uwezeshaji katika Career Fairs na Motisha kwa Shule Kuu ya Biashara,” alisema Prof. Nelson.