Wazalishaji na Waingizaji bidhaa nchini watakiwa kulinda Uchumi wa Taifa

Wazalishaji na Waingizaji bidhaa nchini watakiwa kulinda Uchumi wa Taifa

General / 26th November, 2022

Mkaguzi wa kitengo cha Bidhaa zinazotoka nje ya nchi (TBS), Bw. Andalalisye Mwakyonde amewataka Wazalishaji na waingizaji wa bidhaa kushirikiana na taasisi za serikali ikiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika kuhakikisha kuwa ubora wa bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa nchini unazingatiwa ili kusaidia kulinda uchumi wa nchi na kupunguza hasara kwa wafanyabiashara.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Makao  Makuu ya TBS Ubungo  Jijini Dar es Salaam.

Amesema TBS inafanya ukaguzi mipakani na Bandarini ili kuhakikisha bidhaa zote zinakidhi usalama na ubora uliowekwa, hivyo amewataka waingizaji wa bidhaa kufuata taratibu zote pindi wanapotaka kuingiza bidhaa nchini.

"Shirika la Viwango Tanzania lina kampuni tano zinazofanya ukaguzi katika maeneo ya uzalishaji mkubwa wa bidhaa zinazoingizwa nchini ikiwa ni pamoja na CCIC Intertek , Bureau Veritas, SGS pamoja na TUV walioanza shughuli za ukaguzi mapema Agosti mwaka huu". Amesema

Kwa upande wake Afisa Usalama wa Chakula Mkuu TBS, Bi. Coletha Sarimbo amesisitiza umuhimu wa usajili wa bidhaa hususani za chakula na vipodozi katika kuhakikisha ubora na usalama wa bidhaa husika ili kulinda afya za watumiaji na vilevile kusaidia wananchi kupata taarifa sahihi ya bidhaa kulingana na viambata vilivyopo kwenye bidhaa hizo.

Bi.Sarimbo ametoa wito kwa wafanyabiashara wanaoandaa matangazo yanayohusu vyakula na vipodozi kuyawasilisha TBS kwa ajili ya mapitio na baadae kupewa kibali ili kuhakikisha matangazo hayo hayamrubuni mlaji.