Watoa Huduma za Kifedha Nchini Wametakiwa Kuangalia Upya Masharti ya Mikopo

Watoa Huduma za Kifedha Nchini Wametakiwa Kuangalia Upya Masharti ya Mikopo

General / 24th November, 2022

04%20(1)


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia viongozi na washiriki mbalimbali wakati wa Ufunguzi wa Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa inayofanyika katika Viwanja vya Rock City Mall Jijini Mwanza.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa watoaji wa huduma za kifedha nchini kutazama upya masharti ya mikopo, ikiwemo dhamana ya mali zisizohamishika kwa kuwa ni kikwazo kwa wajasiriamali pamoja na kutafuta njia za kibunifu katika kuwafikia  vijana hapa nchini ili waweze kupata mikopo itakayoinua maisha yao na uchumi wa taifa kwa ujumla.


Makamu wa Rais amesema hayo leo Nov 24, 2022 wakati akifungua Maadhimisho ya Pili ya  Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Rock City Mall Jijini Mwanza. Aidha amesema Riba ya mikopo ya wastani wa asilimia 16 bado ni mzigo kwa Watanzania walio wengi hivyo amesisitiza kila benki kupitia umoja wao (TBA) kuchambua mizizi ya changamoto hiyo na kupunguza zaidi riba kwa wakopaji. 


Aidha, ametoa wito kwa watoaji wa huduma za kifedha nchini kupunguza gharama za kutuma na kupokea pesa kimataifa kwa kuwa zimekua zikisababisha wageni pamoja na diaspora kutumia njia zisizo rasmi wanapowatumia pesa jamaa zao hapa nchini. Ameongeza kwamba kwa upande wa credit cards, tozo za benki na mawakala wao zimekuwa  mzigo na hivyo kukwamisha watalii kununua vitu kwa wingi na kuikosesha mapato Serikali na watoa huduma mbalimbali. 05


Pia ameutaka Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) kusaidia kuhamasisha wanachama wao kutanua wigo wa huduma za kifedha katika maeneo ya  vijijini pamoja na mkopeshe zaidi na kukuza akiba ili kupunguza utamaduni wa wananchi kutunza pesa katika mfumo usio rasmi.


Makamu wa Rais ametoa wito kwa Benki Kuu ya Tanzania kutoa elimu na mwongozo kuhusu fursa na hatari zinazoambatana na maendeleo ya wimbi la fedha za kidigitali (Central Bank Digital Currency, cryptocurrencies, bitcoins n.k.)ambayo yanaigusa jamii  hususan vijana na baadhi ya wastaafu wenye kiu ya kuwekeza huko. Pia amewasisitiza Benki Kuu ya Tanzania na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhakikisha watoa huduma wanaheshimu Sheria ya kumlinda mtumiaji wa huduma jumuishi za fedha kwa njia ya simu za mkononi. Amesema riba zinazotozwa na baadhi ya watoa huduma kutokana na mikopo ya muda mfupi ya fedha na muda wa maongezi ni kubwa hivyo wananchi waelezwe makato yao kabla hawajaamua kuchukua mikopo hiyo.


Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Hamad Chande amesema kupitia maboresho yaliofanyika katika sekta ya fedha nchini jumla ya shilingi Trilioni 3.99 imekopeshwa kwa sekta binafsi ikiwa ni ukuaji wa asilimia 19.4, kuchangia ukuaji wa pato la taifa kwa asilimia 4.9 kwa mwaka 2021 pamoja na kuongezeka kwa matumizi ya huduma za fedha kwa njia ya simu kufikia akaunti milioni 33.14.


Chande amesema sekta ya fedha inakabiliwa na changamoto mbalimbali nchini ikiwemo wananchi kutumia huduma za fedha zisizo rasmi kama vile biashara haramu ya upatu , biashara zisizo rasmi kwa njia ya mtandao pamoja na idadi kubwa ya wananchi kutokuwa na uelewa wan kutosha kuhusu teknolojia ya masuala ya fedha.


Awali akitoa taarifa ya Maadhimisho ya Pili ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa , Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Lawrence Mafuru amesema maadhimisho hayo ni utekelezaji wa mpango mkuu wa maendeleo ya sekta ya fedha wa mwaka 2020/2021-2029/2030 ambao umelenga kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha , mitaji ya muda mrefu kulinda watumiaji wa huduma za fedha, kuimarisha sekta ya fedha, kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya sheria , kanuni , taratibu na miongozo katika sekta ya fedha nchini.


Ameongeza kwamba wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa inalenga kuwafikia wadau mbalimbali wakiwemo watumishi wa umma, wanafunzi, wanawake , vijana wajasiriamali wadogo na wa kati,asasi za kiraia pamoja na zile za kidini.