Washindi 12 wajizolea zawadi nono na ‘NMB Bonge la Mpango’

General / 17th April, 2023

Droo ya kwanza ya msimu wa tatu wa Kampeni ya Weka Akiba na Ushinde iitwayo 'NMB Bonge la Mpango - Moto Ule Ule,' ikiwa imefanyika jana tarehe 13 Aprili 2023 na kushuhudia washindi 12 wakijinyakulia zawadi zenye thamani ya Sh. milioni tano, kati ya Sh. milioni 180 zinazoshindaniwa katika wiki 12 za kampeni hiyo.

Katika droo hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Stella Mafuwe ambaye ni mkazi wa Babati mkoani Manyara alijinyakulia bodaboda.

NMB Bonge la Mpango ilizinduliwa Machi 29 mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Paulo Chacha, chini ya kaulimbiu ya 'Moto Uleule - #Hatupoi'. Kauli mbiu hiyo inalenga kuhamasisha uwekaji akiba, kurejesha kwa jamii sehemu ya faida, huku pia ukiwa ni mkakati wa NMB kuendelea kuwa chaguo la kwanza la wateja kwa usalama wa fedha zao pamoja na uhakika wa huduma bora za kibenki.

Mkuu wa Idara ya Mauzo ya Mtandao wa Kibenki wa NMB, Donatus Richard, ndiye aliyechezesha droo hiyo ya kwanza, iliyofanyika Makao Makuu ya NMB, jijini Dar es Salaam, ikisimamiwa na Afisa wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Elibarik Sengasenga, ambaye kwa niaba ya bodi aliipongeza NMB kwa uratibu muri na kukidhi matakwa ya kisheria na kikanuni wakati wa uendeshaji wa droo za kampeni hiyo kwa misimu miwili iliyopita.

Mbali na Stella Mafuwe wa Babati aliyetwaa bodaboda,naye Deocles Mushemo Muganyizi ambaye ni mteja wa NMB Tawi la Kenyatta Road jijini Mwanza, alijishindia pesa taslimu kiasi cha Sh. 200,000, huku washindi wengine 10 wakijinyakulia Sh. 100,000 kila mmoja.

Akizungumza kabla ya droo hiyo kuchezeshwa, Donatus alizitaja zawadi nyingine za kampeni hiyo kuwa ni pesa taslimu Sh. milioni tano, friji la milango miwili, 'smart tv' (inchi 55), 'smartphone' aina ya iPhone 14 Pro Max na Samsung Z-FLIP, pikipiki za mizigo (za matairi matatu aina ya Skylark) na kompyuta mpakato 'laptop' kwa washindi wa kila mwezi na wale wa fainali ya kuhitimisha shindano hilo.