Wanasheria watakiwa kusimamia haki katika utendaji wao.

General / 24th November, 2022

Image

Na Rajabu Msangi 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan amewataka wanasheria kushirikiana na vyama vyao na Wanasheria wa kitaifa kukuza utoaji wa haki na kuzingatia utoaji wa sheria katika jamii. 


Rais Samia ameyasema hayo leo tarehe 24, Novemba 2022 wakati akifungua Mkutano wa 27 wa Jumuiya ya Wanasheria Afrika Mashariki (EALS) jijini Arusha huku akisisitiza ushirikiano kati ya Majaji na Wanasheria katika kutoa huduma bora kwa wananchi. 


"Kunapokuwa na ushirikiano thabiti, kati ya pande hizi mbili ndipo huduma bora zinapoweza kutolewa kwa wananchi ambao wanategemea Wanasheria na Majaji katika kupata haki na Muongozo kuhusu masuala ya kisheria" Amesema Rais Samia.

Aidha Rais Samia amesema ili haki itolewe vizuri ni lazima wahakikishe wanaepuka suala la Rushwa katika utendaji wa kazi. 


"Tulikuwa tunaangalia magereza yetu idadi ya watu, tukakuta waliofungwa kwa makosa na walioko mahabusu ambao hawajafungwa 'almost' idadi ipo sawa, tukagawana timu nendeni kwenye magereza angalieni, wengi wao kesi ni za kubambikiwa, na ndiyo mana mtu ana miaka mitatu yuko gerezani, haendi mahakamani, haulizwi" ameongeza Rais Samia. 


Katika mkutano huo, Rais Samia amewataka mawakili kusimama pamoja kama Waafrika wa Afrika ya Mashariki hasa katika kukabiliana na changamoto za utandawazi, teknolojia na masuala ya ikolojia kwa kufanya kazi kwa pamoja lakini kwa kuzingatia historia, tamaduni na desturi za kila nchi. 


Hata hivyo Rais Samia amekubali maombi ya chama hicho kupatiwa ardhi ya ujenzi wa makao makuu lakini pia kurahisisha ufanyaji wa kazi kwa ushirikiano baina ya mawakili wa nchi wanachama. 


Naye Rais wa Jumuiya ya Wanasheria Afrika Mashariki (EALS), Bernard Oundo ameomba kuboresha mazingira ya mawakili kufanyakazi ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo, kupata ardhi ya ujenzi wa makao makuu.