Wafamasia Watakiwa Kuhakikisha usalama wa dawa

 Wafamasia Watakiwa Kuhakikisha usalama wa dawa

General / 24th November, 2022


Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaid Ali Khamis amewataka wafamasia nchini  kuwa makini na matumizi sahihi ya dawa ili  kuwe na usalama , kwani wengi wao wamekuwa wakifanya tofauti.


"Dawa ni sumu kama isipotumika sahihi, lakini wengi wenu hamtendi haki kabisa katika kuhakikisha usalama wa mgonjwa katika matumizi ya dawa, mmewaachia majukumu haya wasaidizi wenu, na hivyo kuondoa kabisa umuhimu wenu, na mbaya zaidi inahatarisha maisha ya watanzania hata pale ambapo mfamasia yupo, baadhi yenu ndo mmekuwa mstari wa mbele kushauri matumizi ya dawa bila ya cheti wala vipimo, matumizi yasiyofaa ya dawa na kufanya udanganyifu katika ubora wa dawa ikiwemo kubadili tarehe za kuisha matumizi" Amesema Mwanaidi


Naibu waziri Mwanaidi Khamis ameyasema hayo leo Novemba 24,2022  alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa 52 wa wafamasia na wataalamu wa afya nchini, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma


Aidha, Mwanaidi amesema Chama Cha Wafamasia Nchini (PST) kisiwe chama cha kuleta malalamiko tu bali pia kijitokeze na kukemea vitendo viovu vinavyofanywa na wataalamu wenyewe au wale waliopewa dhamana ya kuhudumia katika sekta ya afya hasa katika upatikanaji wa matumizi sahihi ya bidhaa za afya nchini.


Amesema mabaraza na vyombo husika vinatakiwa kuchukua hatua stahiki bila uonevu wala upendeleo pale panapogundulika ukiukwaji wa taratibu unapoelekea kuzorotesha huduma za afya nchini.


"Ni aibu sana wafamasia mpo, Hospitali fedha kwenda kupata dawa ambayo mngeweza kuandaa kwa gharama nafuu. Mashauri mkayafanyie kazi mapendekezo yenu yaliyotolewa" Amesema Khamis.

Mwanaidi  amewaagiza wafamasia na wataalamu wote nchini kuzingatia utaratibu wa serikali katika kusimamia bidhaa za afya iwe kwenye sekta ya umma au binafsi, lakini pia kutoa elimu kwa umma juu ya matumizi sahihi ya dawa.  

Kwa upande wake  Rais wa Chama hicho Ndug. Fadhili Ezekia, amesema ADO Dispensary na Zahanati zisifungwe bali wapatiwe mafunzo ya muda mfupi wakujiendeleza ili waweze kufikia lengo ambalo ni kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma bora.