Wadau watakiwa kufikisha huduma ya afya ya akili kwenye jamii

Wadau watakiwa kufikisha huduma ya afya ya akili kwenye jamii

General / 31st August, 2023

Serikali imewataka wadau kushirikiana kuhakikisha huduma ya Afya ya akili inapatikana na kufika kwenye Jamii ili kutatua changamoto mbalimbali.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati akizungumza na wadau wa Ustawi wa Jamii Agosti 30, 2023 jijini Dodoma.

Waziri Dkt. Gwajima amesema kuna mambo yanayoweza kuathiri afya ya akili kwa makundi yote ikiwemo changamoto za kiuchumi, migogoro ya ndoa unyanyapaa na vitendo vya ukatili ambavyo vimekuwa tishio kubwa lenye kuathiri afya ya akili.

“Tunapozungumza juu afya ya akili, tunamaanisha hali ya kuwa sawa kiakili na kisaikolojia au kutokuwepo kabisa kwa usumbufu wa akili ya mtu, kimawazo, kihisia, na kitabia; uwezo wetu wa kutatua matatizo na kukabiliana na mambo magumu, muunganiko wetu wa kijamii na uelewa wetu wa ulimwengu unaotuzunguka” alisema Waziri Dkt. Gwajima

Aidha amesema matatizo ya Afya ya akili yanasababisha vitendo vya ukatili vinavyoathiri ukuaji wa watoto na kuharibu nguvu kazi katika Taifa kwa siku za usoni.

“Vitendo hivi vimeendelea kutokea katika nchi zote duniani zilizoendelea na zinazoendelea ikiwemo Tanzania ambapo vinasababisha madhara makubwa kwa mtu binafsi, familia, jamii na Taifa kwa ujumla.” amesisitiza Waziri Dkt.Gwajima

Vilevile amesema kuwa suala la mmonyoko wa maadili ni muhimu kuzingatiwa katika jamii na amewaomba wadau kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha Watoto wanapata Malezi na Makuzi kuanzia miaka 0-8 katika vituo na Makao ya kulea watoto ili kuwa katika mstari mzuri wenye maadili na uzalendo kwa nchi yao.

Awali akimkaribisha Waziri Dkt. Gwajima, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Nandera Mhando amesema Wizara imeweka mikakati mbalimbali hasa katika kuhakikisha huduma ya Afya ya akili inapatikana kwa jamii ili kuweza kupunguza changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii kwasasa hasa vitendo vya ukatili.

Naye Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Subisya Kabuje amesema Ofisi hiyo itashirikiana na wadau katika Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha huduma hizo muhimu za Afya ya akili zinawafikia wananchi na kuwasaidia kutafuta changamoto zinazowakabili ambazo nyingi zinapelekea kuwa na vitendo vya ukatili hata watu kujifanyia vitendo vya ukatili wenyewe.

Nao baadhi ya wadau wa Ustawi wa Jamii nchini wamesema huduma za kisaikolojia kwa jamii ni umuhimu ili kisaidia kuwa na jamii yenye ustawi na Maendeleo.