Upanuzi Kiwanda cha Sukari Kilombero wafikia Zaidi ya Dola Milioni 350.

Upanuzi Kiwanda cha Sukari Kilombero wafikia Zaidi ya Dola Milioni 350.

General / 17th February, 2023

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Kituo cha Uwekezaji (TIC) Bw.Maftah Bunini amesema Uwekezaji uliofanywa katika upanuzi wa Kiwanda cha Sukari Kilombero umefikia zaidi ya Dola za Marekani Milioni 350.


Bw.Maftah Bunini – Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Kituo cha Uwekezaji (TIC)

Akizungumza Wakati hafla ya kushuhudia kuwasili kwa shehena ya vifaa na  mitambo itakayotumika katika upanuzi wa Kiwanda cha Sukari Kilombero akimwakilisha Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji jijini Dar es Salaam amesema Serikali imejipanga kuweka mazingira ya kuwezesha wawekezaji kufanya shughuli zao kwa kuweka vivutio mbalimbali ili kukuza uwekezaji nchini.

“Kiwanda cha sukari Kilombero ni moja ya wawekezaji wakubwa ambao wamesajiliwa na kituo cha uwekezaji, kiwanda hiki kimesajiliwa kwa kupewa tena kibali cha kufanya upanuzi wa kiwanda na hili liliweza kuidhinishwa na kamati ya kitaifa ya wawekezaji mwezi oktoba 6, mwaka 2022.”


“Ili Mwekezaji aweze kuwa Mwekezaji Mahiri maalum anatakiwa kuwekeza mtaji wa kuanzia Dola Milioni Milioni 300, Kiwanda hiki kwa upanuzi uliofanyika unasababisha uwekezaji wa kiwanda hiki uwe ni zaidi ya Dola za Marekani Milioni 350 na hivyo kinakuwa na sifa ya kuitwa Mwekezaji Mahiri Maalum ” Amesema Bw. Bunini.

Aidha amesema uwekezaji ni njia moja wapo ya kuzalisha ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja nchini.

“Kwa njia ya Uwekezaji ajira zinaongezeka , kuna manufaa makubwa yatakayopatikana kutokana na upanuzi huu uliofanyika ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira za moja kwa moja “

“Kulingana na uwekezaji huu zaidi ya watu 1,400 wataweza kuajiriwa katika ajira ya moja kwa moja lakini pia kutakuwa na ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 15,000”

Katika hatua nyingine amesema kutakuwa na ongezeko la uzalishaji kwa wakulima ambao miwa yao itanunuliwa na kiwanda hicho cha Kilombero ambapo idadi ya wakulima inatarajiwa kuongezeka mpaka wakulima 15,000.

“Serikali itanufaika kiasi kikubwa kutokana na uwekezaji huu ambapo kiwanda kitaweza kulipa kodi zaidi”

Bw. Bunini ametoa wito kwa wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania na kwamba Serikali imeendelea kuboresha mifumo ya Uwekezaji ili kukuza uchumi wa Taifa.

“Na ndiyo maana tumeboresha mifumo yetu, ikiwa ni pamoja na kuwa na sheria Mpya ya Uwekezaji ya mwaka 2022 na hivi sasa wawekezaji mazingira yameboreshwa zaidi”


Bruno Daniel – Meneja Masuala ya Biashara wa Kampuni ya Sukari Kilombero, 

Kwa upande wake Meneja Masuala ya Biashara wa Kampuni ya Sukari Kilombero,  Bruno Daniel amesema  Mradi huo unatarajia kuongeza uzalishaji wa Sukari kufikia Tani 144,000 na kufanya uzalishaji wa jumla kuwa Tani 271,000 ifikapo mwaka 2024 huku akibainisha gharama za mradi huo kuwa Bilioni 571.


Mrisho S. Mrisho – Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam

Naye Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Mrisho S. Mrisho ameahidi kuendelea kushirikiana na kiwanda cha Kilombero katika kufanikisha  malengo yao kwa kuendelea kushuha vifaa hivyo vitakavyotumika kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda.

“Meli hii imefika jana usiku na tumeanza kazi na leo tutaendelea nayo, kontena zote hizi tunasema ni abnormal zitashuka vizuri kwa usalama” Amesema Mrisho.

“Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Bandari niwahakikishie tutautoa ushirikiano wowote kufanikisha biashara, sisi kama bandari pamoja na kwamba ni lango la uchumi la upatikanaji wa fedha la Taifa hili lakini pia tuna ‘facilitate’ sekta nyingine kama viwanda na sekta nyingine ambazo mizigo yake inapita katika Bandari ya Dar es Salaam ” Ameongeza Mrisho.